HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 31, 2023

KATIBU TAWALA SINGIDA: WAANDISHI WA HABARI KUWENI WAZALENDO KWA KUANDIKA HABARI ZENYE TIJA


Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko (kushoto) akifungua mkutano wa Uhamasishaji wa Program ya Shule Bora kwa Wasimamizi wa vyombo vya habari na Wahariri Mkoa wa Singida uliofanyika leo Januari 31, 2023 wilayani Manyoni mkoani hapa.

 cNa Dotto Mwaibale, Manyoni

 

WAANDISHI wa Habari Mkoa wa Singida wametakiwa kuwa wazalendo kwa kuandika habari zenye tija kwa mkoa na Taifa kwa ujumla.

 

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko  wakati akifungua mkutano wa uhamasishaji wa program ya Shule Bora kwa Wasimamizi wa vyombo vya habari na Wahariri Mkoa wa Singida uliofanyika leo Januari 31, 2023 wilayani Manyoni mkoani hapa.

 

“Waandishi wa habari mnatakiwa muwe wazalendo kwa kuandika habari nyingi za maendeleo ili kuutangaza mkoa wetu na si kuandika zile zinazohusu mabaya tu japo hazikatazwi” alisema Mwaluko.

 

Aidha Mwaluko aliwataka wanahabari kwenda vijiji kuandika habari za uchunguzi ambazo zitasaidia kuibua changamoto za wananchi, watumishi wa afya na kada zingine na kwenye shule ili ziweze kufahamika na kupatiwa ufumbuzi.

 

Katika hatua nyingine Mwaluko alisema licha ya waandishi wa habari kuwa wengi mkoani hapa haridhishwi na utendaji wao na badala yake amewataka wabadilike ili wawe chachu ya maendeleo ya Mkoa wa Singida.

 

Mwaluko alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wanahabri hao kuwa mwaka huu Mkoa wa Singida utafanya maadhimisho ya miaka 60 tangu uanzishwe mwka 1963 hivyo aliwaomba waandike habari mbalimbali njema zitakazoutangaza mkoa kuelekea kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika Oktoba mwaka huu.

 

Meneja Mawasiliano wa Shule Bora,Raymond Kanyambo akizungumzia program hiyo ya shule bora alisema ni program ya Serikali unaofadhiliwa na UKAID wenye lengo la kukuza na kuboresha ufundishaji na ujifunzaji mashuleni ili kuboresha elimu na kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wa kike na wa kiume wanapata elimu bora.

 

‘Program hii ya miaka sita inatekelezwa katika Mikoa Tisa Tanzania Bara yaani Katavi, Rukwa, Dodoma, Singida, Mara, Simiyu, Pwani, Tanga na Kigoma. Mkoa wa Singida ni moja mojawapo ya mikoa ambayo program hiyo ya Shule bora inatekelezwa kwenye shule mbalimbali,"alisema Kanyambo.

 

Kanyambo aliongeza kuwa program hiyo imefadhiliwa na Uingereza kwa Paundi milioni Tisa ,ambapo unaifikia mikoa hiyo ili kuhakikisha watoto wote hata wale wenye changamoto mbalimbali wanapata fursa ya kusoma.

 

Alisema, program hiyo itaweza kuwaendeleza walimu kufundisha kwa ufanisi ili kuinua kiwango cha taaluma mashuleni na kuwa na mazingira bora ya ufundishaji na kuwa imelenga kuiunga mkono Serikali katika kuinua kiwango cha elimu jumuishi pamoja na kuweka mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wote.

 

Aidha, Kanyambo alisema mkutano huo umewashirikisha waandishi wa habari ili kushirikiana nao kutokana na umuhimu wao wa kupasha habari jamii na jinsi ya kuandika habari zinazohusu elimu na changamoto zake na kufanya uhamasishaji wa jamii, wazazi umuhimu wa masuala ya elimu kwa watoto.

 

“Tunahitaji ninyi waandishi wa habari mliopo kwenye halmashauri zote za wilaya kutuunga mkono katika jambo ili muhimu kwani sisi tunafanya kazi na vyombo vyote vya habari bila ya kuvibagua” alisema Kanyambo.

 

Mada kubwa iliyotolewa katika mafunzo hayo ni Mawasiliano ya program na ushiriki wa vyombo vya habari katika kufanikisha malengo ya program hiyo.

 

Mratibu wa Program hiyo Mkoa wa Singida, Samwel Daniel alisema program hiyo inawahusu wanafunzi wa shule za awali na msingi na kuwa walitoa mafunzo endelevu kwa walimu wakuu, mahiri na taaluma ambapo walimu 1774 wamenufaika nayo.

No comments:

Post a Comment

Pages