HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 21, 2023

MBUNGE MSONGOZI AWALETA WAFANYABIASHARA KUTOKA URUSI KUNUNUA KAHAWA RUVUMA


NA STEPHANO MANGO, SONGEA

 

WAFANYABIASHARA wa zao la kahawa kutoka nchini Urusi wanatarajia kununua zao hilo kutoka kwa wakulima wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma baada ya kuridhika na ubora wa kahawa kutoka Wilayani humo.


 

Akizungumza juu ya ujio wa wageni hao Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Jacklin Ngonyani Msongozi alisema kuwa jukumu langu ni kuhakikisha tunafungua milango ya uchumi kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kwenye nyanja zote za kiuchumi ndio maana nimewaleta wafanyabiashara hao kuja kununua zao la kahawa

Msongozi alisema kuwa ugeni huu ulianzia nyumbani kwangu Jijini Dodoma kabla ya kusafiri na kuja Mkoani Ruvuma ambapo wakiwa hapa mkoani Ruvuma ugeni huu ulipokelewa na Mratibu wangu Dkt Denis Mpagaze

“Ninayofuraha kubwa kuwapokea wawekezaji kutoka Nchini Urusi (Russia) ambao kwa juhudi zangu nikiwa mwakilishi wa Mkoa wa Ruvuma nimefanikiwa kuwashawishi kuja nchini Tanzania hususani Mkoani Ruvuma kwa minaajili ya kuja kujionea uzalishaji wa Kahawa na hatimae kuinunua na kuisafirisha kwenye soko nchini Urusi, Dubai, Marekani na nchi zingine za barani Ulaya” alisema Msongozi

Alisema kuwa walipata wasaa wa kwenda kujitambulisha  na kueleza madhumuni yao Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambapo walijitambulisha na kuzungumza na Katibu Tawala wa Mkoa kwa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Afisa Kilimo wa Mkoa na Mrajisi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma

Alieleza zaidi kuwa ujumbe huu baada ya kujitambulisha na mazungumzo mafupi  na Katibu tawala (aliyekua akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa) ulisafiri mpaka wilayani Mbinga ambapo mara baada ya kuwasili moja kwa moja ulikwenda kujitambulisha Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Mji wa Mbinga

Alifafanua kuwa mara baada ya utambulisho huo ugeni huu  ukiwa na wenyeji wetu wa Mbinga ulipata wasaa wa kwenda kutembelea AMCOS, SACCOS, wakulima wakubwa wamiliki wa viwanda na makampuni mengine yanayojihusisha na uzalishaji na uuzaji wa kahawa.

Akizungumza mafanikio ya ziara ya wafanyabiashara hao Mwakilishi wa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Dkt Denis Mpagaze alisema kuwa wafanyabiashara hao wamechunguza kwa kina ubora wa zao la kahawa ambayo inazalishwa Wilayani Mbinga na kwamba wameridhika kuanza kuinunua baada ya  ya taratibu za kisheria kukamilika

Dkt Mpagaze alisema kuwa taratibu zote za kisheria na za kinchi zitafuatwa ikiwemo kuingia mikataba ambayo itafungua rasmi milango ya ununuzi wa Kahawa.

Kwa upande wake Onesmo Ngao ambaye ni Afisa Kilimo Mkoa wa Ruvuma alimpongeza Mbunge Msongozi wa kuwaleta wafanyabiashara hao ambao watatanua wigo wa biashara ya kahawa kutoka Mkoani Ruvuma

No comments:

Post a Comment

Pages