HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 25, 2023

BENKI YA CRDB YAFUNGUA MILANGO KWA WABUNIFU NCHINI

NA JOHN MARWA

BENKI ya CRDB inawakaribisha wabunifu wote nchini kwenye benki hiyo na taasisi zao za CRDB Benki Foundation katika safari ya kukuza biashara zao.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mikopo Benki ya CRDB, Xavery Makwi katika hafla ya kufunga mafunzo ya wabunifu wa Programu ya Imbeju iliyoandaliwa na benki ya CRDB yenye lengo la kutoa mtaji wezeshi kwa vijana na wanawake.



“Nichukue fursa hii kuwakarisbisha wabunifu wote nchini katika Benki ya CRDB na taasisi zetu za CRDB Benki Foundation katika safari ya kukuza biashara zao.

“CRDB Benki inahimiza sana ugunduzi, kama Benki tuna kitengo cha wagunduzi vijana waliosoma, wakike na wakiume wanabuni mambo, hata hii simbanking iliyoboreshwa ni matokeo ya vijana wabunifu waliokaa wanafikilia na kufanya kazi vizuri kweli kweli. Kwahiyo hata wabunifu watakao pita kwenye Programu hii ya Imbeju tunaimani watafanya kazi kubwa sana kwa ajili ya Tanzania” Amesema Xavery Makwi na kuongeza kuwa.

“Mada zilizowasilishwa hapa kwa wiki nzima sio kwamba zimetosha kuwafanya kuwa wajasiriamali mliokamilika bali zimewasugua ubongo kwa tamaa ya kutaka kujifunza zaidi na kuwa bora kuliko mlivyokuja hapa.

“Wiki moja ya kukaa kwenu hapa sio kwamba imeisha bure bali mmejenga msingi wa mawasiliano yatakayo wawezesha kubadilisha uzoefu na kuimarisha mtandao wa biashara changa ambazo ni muhimu kwa msingi wa biashara kote nchini” amesema Makwi na kubainisha kuwa.

“Hatua itakayofuata baada ya kambi hii ya mafunzo ni tathimini ya maombi mliyowasilisha. Tumeandaa utaratibu bora wa kuwasiliana nanyi na kuwapa nafasi ya mtu mmoja mmoja kukutana na wataalamu wetu ili kufahamu zaidi kuhusu miradi yenu na kuwashauri ipasavyo. Mchakato huo utaanza tarehe 3 julai.

“Mchakato huu wa kuwasiliana na kushauriana ni muhimu sana kwani mfanyabishara ndiye anaye fahamu vizuri wazo lake la biashara. Tunaamini mtakuwa mabalozi wazuri kwa manufaa ya uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.

“Benki ya CRDB ni moja kati ya taasisi za fedha ambazo zinaipa uzito mkubwa suala la uwezeshaji kwa vijana na wanawake ambayo kwa miaka mingi imekuwa ni huduma mahususi kwa ajili yao na kutambua haya ni makundi yenye umuhimu wa kipekee ndio maana tukaja na Programu hii ya Imbeju mahususi kwa ajili yenu." Amesema Makwi.

Wakitoa neno la shukrani baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo baadhi ya washiriki wameahidi kufanya vizuri ili kuwa mabalozi wa mfano katika jamii na taifa kwa ujumla kwa manufaa ya kesho na baadae.


“Tunashukura sana CRDB Benki kwa nafasi hii ya kipekee sana, Mbegu hii tuliyopewa ni mbegu ya biashara ni mbegu ya maisha kutoka kwa watu wote waliotufundisha. Tumefahamiana na naamini tutaenda kufanya biashara kwa pamoja, tumeona kwa pamoja sisi wabunifu na wafanyabishara tunaweza kufanya kazi pamoja.

“Lakini pia tunaomba tuahidi kwamba mbegu hii tunayoenda kuipokea tutaitunza. Sisi tunaahidi tutaenda kuitunza , tutaenda kuizalisha, lakini pia itaenda kuleta tija.

"Naomba niongee na wabunifu wenzagu tuna namna mbili tunaweza kutolea mifano , unaweza kuwa mfano kwamba wewe umefanya kitu bora lakini naomba tukawe mfano wa kufanya kazi bora na kutengeneza njia kwa ajili ya wengine watakaofuata.” Amesema Raphia Kimaro mshiriki wa Programu ya Imbeju.

“Sijui jinsi gani tutawashukuruni kwa sababu mmegusa panapouma. Sisi ni kama yatima wanao landalanda mitaani wasio kuwa na mlezi, tunakuwa na malengo lakini tunahitaji wakutushika mkono na kutuongoza kuweza kufika.

“Sote tuna mitazamo chanya kwenye ugunduzi na uvumbuzi juu ya biashara mbalimbali ambazo tunajiwekeza kupambana nazo. Nasi tunatamani kuweza kukua na kuwa na uwezo wa kuajili watu zaidi ya 1000 kama nyie CRDB.


"Tuna nafasi ya kukua katika njia hiyo, tukipewa nafasi na sapoti ambayo tunahitaji kutoka kiwango cha chini tutakuwa kibishara na kuwa na makampuni makubwa.” Amesema Mohamed Awami mshiriki wa Programu ya Imbeju.

 
 

Kufungwa kwa mafunzo hayo kumeambatana na ugawaji wa vyeti kwa Washiriki hao ambao ni kati ya wabunifu 709 waliotuma maombi yao kuanzia Machi 12 Program hiyo ilipozinduliwa na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) na kukidhi vigezo vya awali vilivyowekwa.

No comments:

Post a Comment

Pages