Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera (kushoto) na Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi na Mauzo wa Benki ya NMB, Donatus Richard, wakipeperusha Bendera kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya Onja Unogewe kwa kanda ya nyanda za juu inayolenga kuhamasisha matumizi ya kufanyia malipo kwa njia ya kidigitali kupitia NMB Lipa Mkononi inayoendeshwa na Benki hiyo katika stendi ya mabasi madogo ya nane nane jijini Mbeya.
NA MWANDISHI WETU, MBEYA
MKUU wa Mkoa (RC) wa Mbeya, Juma Homera, amezindua rasmi Kampeni ya NMB Onja Unogewe inayoendeshwa na Benki ya NMB chini ya Mwamvuli wa Teleza Kidigitali, inayohusisha malipo kwa njia ya QR Code kwa usalama wa pesa za wafanyabiashara na wanunuzi, lengo likiwa kuhamasisha mhamo wa jamii kutoka kwenye matumizi ya pesa taslimu kwenda katika matumizi yasiyo ya pesa taslimu (cashless).
Uzinduzi huo umefanyika katika Viwanja vya Stendi ya Daladala ya Nanenane jijini hapa, ambapo RC Homera aliipongeza NMB kwa wazo zuri lililozaa huduma rahisi, nafuu na salama, ikianikizwa na jina la Kampeni lenye mvuto, msukumo na nguvu ya ushawishi katika kubadili mitazamo ya watu kwenye suala zima la huduma jumuishi za kifedha.
Akizungumza katika uzinduzi huo, RC Homera aliishukuru NMB kwa kuzindulia Kampeni hiyo jijini Mbeya, moja ya mikoa ya mpakani ambayo inakabiliwa na matukio mengi ya wizi, ujambazi na upotevu wa pesa, huku akiwataka wakazi wa Nyanda za Juu kuchangamkia QR Code za benki hiyo ili kukabiliana na changamoto hizo katika mauzo na manunuzi yao ya kila siku.
RC Homera, ambaye aliita NMB kuwa 'nyumba ya ubunifu' kutokana na kushamiri kwa bunifu za kihuduma zinazotoka suluhishi mbalimbali za kifedha, aliwahimiza Wana Mbeya kuachana na tamaduni za kutembea na pesa mifukoni ama kuhifadhi fedha majumbani, badala yake wajiunge na NMB kwa ustawi wa akiba zao na wepesi katika kuhudumiwa kidigitali.
"Wana Mbeya - hasa watoa huduma za bajaji, bodaboda, mama lishe, wauza maduka, wafanyabiashara, wajasiriamali, mnapaswa kuchangamkia huduma hii. Wekeni QR Code hizi madukani na sehemu zenu za biashara, kuwawezesha wateja kufanya malipo na kuepukana na mtukio hatarishi kwa fedha zao yanayoikabili jamii, hususani mikoa hii ya mipakani.
"Tumepakana na Zambia na Malawi, hali inayotuweka jirani na wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka nchi hizo kuja Tanzania kupitia Mbeya, hivyo watapoingia na kukuta QR Code za NMB, itawarahisishia malipo na watavutiwa kuja kwa wingi na kununua na kulipa fedha kwa kadi zao. Ndio maana nasema suluhishi hii ya Onja Unogewe ni huduma bora na rafiki kwa wanunuzi na wauzaji," alisema RC Homera
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard, alisema licha ya Onja Unogewe kubeba dhana nzima ya suluhu za kifedha katika manunuzi na malipo, pia Kampeni hiyo inawapa fahari wao kama benki - kwamba wanasapoti dhamira ya Serikali katika kujenga Mfumo Jumuishi wa Masuala ya Fedha kupitia mapinduzi ya kidigitali waliyoyafanyia uwekezaji mkubwa.
Donatus alibainisha ya kwamba benki yake inajivunia sana bunifu za suluhishi za kifedha, alizozitaja kuwa ndio siri ya mafanikio ya benki hiyo, ambayo mwaka jana iliuongezea thamani Mwamvuli wa Teleza Kidigitali ulioanzishwa mwaka 2019 kwa kuizindulia Huduma ya NMB Pesa Wakala - ambayo ni maalum ya kuweka na kutoa pesa kirahisi kupitia mawakala wanaotumia simu za mkononi.
"NMB Onja Unogewe ni maboresho ya Huduma ya Lipa Mkononi 'QR Code,' ambayo inaenda kumpa wigo mpana mteja wa kulipia huduma kwa njia ya kidigitali, ambako atanufaika na rejesho la asilimia 10 katika malipo yake. Tunafanya hivyo kwa makusudi ili kuvutia zaidi watumiaji wa huduma zetu za kimtandao ili kupunguza matumizi ya pesa taslimu.
"Pamoja na suluhishi hizi zote tunazobuni, kuzindua na kuzitoa kwa Watanzania, ikiwamo mikopo nafuu isiyo na masharti ya Mshiko Fasta, bado tuna utamaduni endelevu wa kurejesha kwa jamii katika sekta za elimu, afya na mazingira.
"Tupo katika Kampeni Endelevu ya Upandaji Miti Milioni 1 mwaka huu wa iliyozinduliwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango jijini Dodoma, huku tukitoa misaada mbalimbali kupitia Mwamvuli wa Program ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR)," alisema Donatus na kuongeza kuwa ahadi yao kama benki ni kuendelea kuisapoti Serikali katika utatuzi wa changamoto za kijamii.
No comments:
Post a Comment