HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 23, 2024

Dkt. Nchimbi: CCM inatambua mchango Wazee


KATIBU Mkuu wa CCM Taifa Balozi Emmanuel Nchimbi,akiwahutubia Mabaraza ya Wazee wa CCM Mkoa wa kusini na Kaskazini Pemba katika ukumbi wa Makonyo Wilaya ya Chake Chake.

 

 

NA IS-HAKA OMAR, PEMBA

 

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi, amesema maendeleo yaliyofikiwa nchini yametokana na juhudi kubwa za kiutendaji zilizoasisiwa na Wazee wa Chama hicho waliohudumu kwa bidii na maarifa katika sekta za umma na binafsi.

 

Kauli hiyo imeitoa katika ziara yake siku moja wakati akizungumza na kujitambulisha kwa Mabaraza ya Wazee wa CCM wa Mikoa ya Kaskazini na Kusini Pemba huko ukumbi wa Makonyo.

 

Balozi Dkt. Nchimbi, alisema CCM inaendelea kuimarika kisiasa, kijamii na kiuchumi kutokana na misingi mizuri iliyowekwa na Wazee wa Chama hicho enzi za utumishi wao toka walipoviunganisha Vyama vya ASP na TANU na kuzaliwa kwa CCM mwaka 1977.

 

Alisema wazee hao wamefanya kazi kubwa ya kuasisi Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa mwaka 1964 kwa dhamira za kuikomboa nchi kutoka katika mikono ya kisultani na kikoloni.

 

Katika maelezo yake Dkt.Nchimbi, alisema kuwa CCM inatambua mchango mkubwa wa wazee wa Chama hicho kwa juhudi zao kubwa za kuitumikia nchi kwa uadilifu jambo ambalo ndio kielelezo cha kifikia maendeleo endelevu yalipo nchini.

 

Alisema lengo la ziara hiyo ni kukutana na wazee hao ili kubadilishana nao mawazo pamoja na kusikiliza changamoto,ushauri na mapendekezo yao juu ya kuimarisha masuala mbalimbali ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

 

“Tunathamini juhudi zenu kwani enzi zenu mlitumikia nchi kwa juhudi kubwa mkaanzisha Chama Cha Mapinduzi na kuweka misingi imara inayotuongoza hadi hivi sasa hivyo nakuombeni muendelee kutushauri na kutuelekeza pale mtakapoona tunaenda kinyume na misingi hiyo”,alisema Dkt.Nchimbi.

 

Balozi Dkt.Nchimbi,alikemea vitendo vya ubaguzi wa kiitikadi,kidini na kikabila na kwamba vitendo visipokemewa vinaweza kuingiza nchi katika machafuko ya kisiasa.

 

Katibu Mkuu huyo Dkt.Nchimbi,alipongeza hatua kubwa ya mafanikio iliyofikiwa na Serikali ya awamu na nan echini ya Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi katika nyanja za kisiasa,kiuchumi na kijamii.

 

Pamoja na hayo aliwasihi Wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ili afikie maono ya kuongoza nchi kwa ufanisi zaidi.

 

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amesema kupitia kitabu cha taratibu za sehemu ya wazee wa CCM toleo la 2019 ibara ya 10(2) inafafanua kuwa wazee ni hazina kubwa ya busara,hekima,uzoefu wa kuendesha shughuli za Chama na maendeleo ya nchi.

 

Dkt.Dimwa,alieleza kuwa CCM Zanzibar ipo imara na itaendelea kutekeleza siasa za kistaarabu zinazozingatia ushindani wa sera kwa vitendo huku ikijipanga kuhakikisha inashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

 

Kwa upande wake Katibu wa Wazee wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba,Bi.Hanuna Ibrahim Masoud,amesema wamefurahishwa na uteuzi wa Katibu Mkuu huyo wa CCM Dkt.Nchimbi kwani ni kiongozi mchapakazi,mbunifu,mzalendo na anayekijua vizuri Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake.

No comments:

Post a Comment

Pages