Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa kikao na Ujumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Burundi ikiongozwa na Waziri wa Miundimbinu na Makazi, Mhe. Dieudonne Dukundane (hayupo pichani), ambapo wamejadiliana kuhusu ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) itakayounganisha nchi hizo mbili ambayo itachochea shughuli za kiuchumi. Kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma, kimehudhuriwa pia na Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Leontine Nzeyimana, Mkurugenzi wa Mipango na Usanifu kutoka Wizara ya Miuondombinu na Makazi Burundi, Mhandisi Pasteur Bisekere, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni Bw. Japhet Justine (wa kwanza), Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. Robert Mtengule, Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. James Msina na Mchumi kutoka Idara ya Fedha za Nje, Bw. Frank Mangap.
Na Joseph Mahumi na Josephine Majura, WF, Dodoma
WAZIRI
wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekutana na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Miundombinu wa Burundi Mhe. Dieudonné Dukundane,
kuhusu maendeleo ya Mradi wa Reli ya Kisasa SGR utakaoziunganisha nchi
hizo mbili.
Katika
mazungumzo hayo yaliyofanyika Dodoma, Viongozi hao wamesema kuwa mradi
huo utakapokamilika utachochea biashara ya madini na kilimo pamoja na
kuimarisha mahusiano ya kikanda na kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
Dkt.
Nchemba alisema kuwa Ushirikiano wa nchi hizo mbili katika maandalizi
ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) umekua mzuri na kwamba watalaamu wa
pande zote mbili wameendelea na vikao hususan katika eneo la manunuzi na
fedha ili kuhakikisha kila kitu kinafanikiwa.
“Ujenzi
wa Reli hii ya Kisasa ya kuunganisha nchi zetu ni muhimu sana kwetu na
maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Samia Suluhu Hassan, kuwa ni mradi wa Kipaumbele na anataka ukamilike”
aliongeza Mhe Dkt. Nchemba
Alisema
kuwa wataalum kutoka nchi hizo mbili wanaendelea kushirikiana ili
kuhakikisha kila kitu kinafanikiwa na kufikia matarajio ya Rais wa
Tanzania pamoja na Rais wa Burundi ya kuona mradi huo unafanikiwa.
Naye
Waziri wa Miundombinu na Makazi wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Dieudonné
Dukundane, alisema kuwa nchi yake itahakikisha kuwa mradi huo unapewa
kipaumbele na tayari timu ya wataalam kutoka Burundi ipo Dar es Salaam
ikiendelea kupitia masuala ya manunuzi wakishirikiana na wataalam wa
Tanzania.
“Rais
wangu Mhe. Evariste Ndayishimiye, ametuelekeza kuwa tufuatilie kwa
ukaribu na kwa kipaumbele mchakato mzima unakwenda kama ilivyopangwa ili
uishe vizuri, na mimi nimeishi hapa Tanzania kwa miaka sita (6) nimeona
namna ambavyo SGR itakavyoharakisha maendeleo ya nchi” alisema Mhe.
Dukundane.
Mradi
huo wa Reli ya Kisasa (SGR) baada ya kukamilika hususan Ujenzi wa Reli
ya Uvinza hadi Musongati nchini Burundi kutawezesha kusafirisha tani
milioni 3 za madini kwa mwaka kutoka mgodi mkubwa wa madini ya Nickel
uliopo Musongati nchini Burundi unaokadiriwa kuwa na hifadhi ya tani
milioni 150 za madini ya Nickel, Cobalt na Copper, na pia kuimarisha
shughuli za kiuchumi za nchi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment