Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TEF, Neville Meena, akizungumza katika mkutano huo.
Wahariri wakiuliza maswali.
NA MWANDISHI WETU, DAR
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imeeleza mafanikio iliyopata katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, huku ikisema siri ya mafanikio hayo ni juhudi za Rais huyo wa Awamu ya sita kutangaza utalii kupitia Filamu ya The Royal Tour.
Kutokana na juhudi za Rais, Dk. Samia kutangaza utalii na vivutio vya ndani kupitia The Royal Tour, kutoa fedha za kuendeleza miundombinu ya utalii na fursa za kutangaza katika masoko ya Kitaifa na Kimataifa, TAWA imesema idadi ya Watalii wa Picha na Uwindaji, imeongezeka kutoka mwaka 2021 hadi Februari 2024.
Mafanikio hayo na mengineyo yamewekwa hadharani na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda, wakati wa mkutano wa mamlaka hiyo na Wahariri wa vyombo vya Habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), lengo likiwa kuishirikisha kada hiyo muhimu katika taarifa ya mafanikio kwa miaka mitatu ya Rais Samia.
Akizungumza na Wahariri hao na wawakilishi wao, Nyanda alibainisha kuwa amekutana na wahariri hao kutokana na kutambua umuhimu na nafasi ya vyombo vya habari katika kuendeleza uhifadhi wa rasilimali ya wanyamapori na shughuli za utalii nchini na hivyo kuchangia katika juhudi za kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.
“Ndugu Wahariri, kutokana na juhudi za Rais Samia, kupitia Filamu ya The Royal Tour, fedha za kuendeleza miundombinu ya utalii na fursa zake, mafanikio mengi na makubwa yamepatikana, ikiwemo Idadi ya Watalii wa Picha na Uwindaji.
“Idadi yao imeendela imeongezeka kama ifuatavyo: Watalii wa Picha waliotembelea vivutio kutoka 37,684 mwaka 2020/21 hadi 166,964 (2022/23) na watalii 116,529 hadi Februari 2024, huku Wawindaji idadi yao ikipaa kutoka 355 mwaka 2020/21 hadi wawindaji 787 (2022/23) na wawindaji 481 hadi Februari mwaka huu.
“Pia, kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya meli za Kimataifa za utalii kutembelea Eneo la Kihistoria la Kilwa, kutoka meli nne zilizokuwa na watalii 400 mwaka 2020/21, hadi meli nane zenye watalii 925 Februari 2024,” alisema Nyanda katika mkutano huo.
Alibainisha kuwa, miongoni mwa matunda ya Filamu ya The Royal Tour ni mwitikio wa mkubwa wa wawekezaji katika mnada wa vitalu vya utalii, ambapo jumla ya vitalu 66 vimeuzwa na mapato ya jumla ya Dola za Kimarekani 8,277,000 zilikusanywa.
Kamishna Nyanda alifafanua kuwa, kiasi hicho ni kulinganishwa na Dola 2,405,000 endapo vitalu hivyo vingeuzwa kwa njia ya utawala, ikiwa ni ongezeko la Dola 5,872,000 za Kimarekani.
“Serikali ilikamilisha taratibu za uwekezaji kwa ajili ya kusaini mikataba ya uwekezaji mahiri katika Vitalu vya Ikorongo, Grumeti, Maswa Mbono, Maswa Kimani, Maswa North, Mkungunero na Selous LL1.
“Mikataba saba ilisainiwa Januari 2024 ambapo kupitia mikataba hiyo Serikali itapata Dola za Marekani milioni 312. 25 kwa kipindi cha miaka 20, sawa na wastai wa Dola za Marekani milioni 15.5 kwa mwaka na kutokana na juhudi hizo, idadi ya vitalu vya uwindaji vyenye wawekezaji imeongezeka kutoka kutoka 59 hadi 68.
“Kusainiwa na kuanza utelelezaji wa Mikataba ya Uwekezaji Mahiri (SWICA), jumla ya Dola za Marekani 2,773, 000 (sawa na Sh. Bilioni 7.01) zimekusanywa tangu kusainiwa kwa mikataba yake, Januari 3 mwaka 2024,” aliongeza Kamishna Nyanda.
Kuhusu Kuimarika kwa Miundombinu ya Utalii, Kamishna Nyanda aliwaambia Wahariri hao kuwa kwa kutumia fedha zilizotolewa kwa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 (TCRP), Miundombinu Wezeshi ya Utalii katika maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka imeboreshwa.
“Kupitia uimarishwaji huo, miradi mbalimbali imetekelezwa, ikiwemo kujenga kilomita 431.4 za barabara katika Mapori ya Wamimbiki, Mpanga Kipengere, Igombe, Swagaswaga, Mkungunero, Kijereshi, Rungwa na Pande, pamoja na ukarabati wa viwanja vya ndege vitatu (3) katika mapori tengefu.
“Hapa namaanisha Mapori Tengefu ya Lake Natron (Engaresero) na Pori la Akiba Maswa (Buturi na Mbono), ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kupumzika wageni (Bandas 13, Campsites - 6, picnic sites - 8, lounge 1) na hosteli moja katika Mapori ya Akiba Mpanga Kipengere.
“Mapori mengine ni pamoja na Mkungunero, Lukwika Lumesule, Pande Swagaswaga na Magofu ya Kilwa na ndio maana tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa kuendelea kutuamini na kutupatia fedha za kuboresha miundombinu hii ya utalii,” alibainisha Kamishna Nyanda katika hotuba yake.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TEF, Neville Meena, aliipongeza TAWA kwa mafanikio mbalimbali iliyoainisha katika mkutano huo, huku akikiri kwamba yeye ni shuhuda wa baadhi ya maboresho ya miundombinu katika Sektas ya Utalii na Mapori ya Akiba kadhaa aliyowahi kutembelea
Akashauri wanyamapori waelimishwe ili kupunguza migogoro inayoepukika baina yao na wananchi, kwani baadhi ya binadamu wana hulka za udikteta, wakiwemo baadhi ya askari hao, ambao wakivaa sare za kazi wanapiga raia kwa kisingizio cha kupambana na ujangili.
“Jukumu lao ni kulinda wanyamapori dhidi ya majangili, lakini sio kupiga ovyo wananchi ambao sio wahalifu, mamlaka zijikite katika kuwaelimisha zaidi ili kuepukana na migogoro inayoepukika.
“Pia, matumizi ya vyombo vya habari, yatasaidia kufikisha elimu kwa wananchi, TAWA iwaoneshe na kuwafichua wananchi wanaovamia na kujenga uzio wa maeneo yao na kuwazuia wanyamapori kukosa haki zao za kimsingi zilizoko hifadhini/mbugani,” alisema Meena.
Kuhusiana na changamoto ya wanyama waharibifu na wakali kama tembo kuvamia makazi na mashamba ya wananchi, Meena alishauri Mamlaka hiyo kuweka mpango mkakati wa kuzilinda njia kuu za Wanyama hao ‘shoroba’ ili kuepusha taaruki za uvamizi huo.
“Kufanya hivyo kutaepusha bomoa bomoa kuhamisha makazi ya watu wanaovamia mapori tengefu na yale ya akiba. TAWA mmeaminiwa na Serikali, lindeni shoroba za Wanyama kutovamiwa na wananchi, ili kulinda Wanyama na kuheshimu njia zao ambazo rekodi zinaonesha wanaweza kuzipita hata baada ya miaka 10,” alisema.
No comments:
Post a Comment