HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 20, 2024

DC Mtambule atoa somo OSHA

Na Selemani Msuya

WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), umetakiwa kuwa wakali na kuhakikisha sheria, taratibu na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi zinazingatiwa na waajiri na wawekezaji wanaowekeza nchini.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule wakati akifungua mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa na OSHA kwa ajili ya wahariri wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), zaidi ya 50 ambayo yalilenga kuwaelimisha kuhusu majukumu ya taasisi hiyo ya umma.

Mtambule amesema OSHA imekuwa ikifanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake, ila inapaswa kuongeza kasi katika kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zanafutwa, ili kuhakikisha utatu wanaousimamia unafanya kazi kwa ufanisi.

“Tumeona kasi ya wawekezaji kutoka nje na ndani kuwekeza nchini, ila uwekezaji huo utakuwa na tija iwapo sheria, kanuni na taratibu za usalama na afya mahali pa kazi zitazingatiwa na wawekezaji hao na hilo linaweza kuonekana iwapo OSHA itatekeleza majukumu yake kwa weledi,” amesema.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan anapambana kila kukicha kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji, lakini haitakuwa na maana iwapo kutakuwa na ukiukwaji katika eneo la usalama na afya mahali pa kazi.


Mtambule amesema Kinondoni kuna zaidi ya viwanda 150 na taasisi nyingine za umma na binafsi, hivyo kuiomba OSHA kuongeza kasi ya ukaguzi ili kuweza kuchukua hatua iwapo kuna vitendo vya ukiukwaji kwa mujibu wa sheria wanayosimamia.

Amesema uamuzi wa OSHA kutoa mafunzo kwa wahariri na waandishi ni ushahidi tosha kuwa taasisi hiyo inahitaji jamii hasa iliyopo kwenye ajira inatambua majukumu yao na kuwaomba waandishi wazingatie sheria, maadaili na misingi ya kazi zao katika kuelimisha jamii.

Awali akimkaribisha mkuu wa wilaya kufungua mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kwa kundi hilo la wahariri, ili liweze kujua majukumu yao na kusaidia kuhabarisha umma kwa ufasaha.

“Tumewaita wahariri ili wajue OSHA inafanya nini, kwanini serikali ilianzishwa, kwani usalama na afya mahali pa kazi, tunaamini wakielewa na kuongea, tunakuwa tumeongea sisi. Kundi hili linakutana na waajiri na wafanyakazi, hivyo kupitia mafunzo haya ya mara kwa mara ni imani yetu kutakuwa na mabadiliko chanya,” amesema.

Amesema mafunzo hayo yamejikita katika sheria ya usalama na afya mahali pa kazi, vihatarishi vya sehemu za kazi na maeneo mengi ambayo yanahusiana na eneo lao.

Mwenda amesema mipango na mikakati ya OSHA ni kuona uchumi wa nchi na wananchi utakuwa, hali ambayo itatoa tafsiri sahihi ya jitihada za Rais Samia kuvutia wawekezaji.

Mtendaji Mkuu huyo amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani OSHA ilikuwa imesajili sehemu za kazi 360 ila ndani ya miaka mitatu wameweza kusajili zaidi ya sehemu za kazi 11,000 jambo ambalo linatoa tafsiri kuwa kuna mabadiliko chanya ya kiuwekezaji.

Mwenda amesema ofisi yake itajipanga kuhakikisha wahariri na waandishi wa habari wanapata nafasi ya kutembelea maeneo ambayo yamesajiliwa ili kuona kivitendo mambo ambayo wanayakagua.

Mtendaji huyo amezitaka taasisi zote za umma na binafsi kuhakikisha zinasajili maeneo ya kazi kama sheria inavyotaka na kwamba hawamvumilia mwajiri ambaye anashindwa kusajili taasisi yake.


Akizungumza kwa niaba ya wahariri, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TEF, Salim Said Salim amesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwao na kuahidi kuwa mabalozi wa kweli kwa OSHA.



No comments:

Post a Comment

Pages