Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amepongezwa kwa kuwakutanisha wananchi wa jimbo lake kusheherekea nao Siku Kuu ya Eid El Fitri jambo lililoelezwa kuwa linaleta umoja na ushirikiano kwenye jimbo hilo.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 11 April 2024 wakati wa Eid pili katika hafla iliyoambatana na chakula cha mchana iliyofanyika nyumbani kwake Kibaoni halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele na kujumuisha watu mbalimbali akiwemo Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaji Majid Mwanga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Mwariko pamoja viongozi wa dini kutoka misikiti 19 ya jimbo la Kavuu.
Wakizungumza wakati wa hafla hiyo, viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini walitoa pongezi kwa Mbunge huyo wa Kavuu kwa uamuzi wake wa kuwakutanisha waumini wa dini ya kiislamu na wananchi wengine kwa ajili ya kusherekea siku kuu ya Eid El Fitri.
Wamesema, katika historia ya jimbo hilo la Kavuu hiyo ni mara ya kwanza kufanyika hafla ya aina hiyo ambapo wameielezea kuwa, siyo tu iimeleta umoja na ushirikiano bali imeleta faraja kwa wananchi kwamba mbunge wao yuko karibu nao.
Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaji Majid Mwanga amesema, watumushi wa umma katika wilaya yake wanayo faraja kubwa ya kuwa na mbunge katika hafla ya kusheherekea siku kuu ya Eid pamoja ambapo ameweka bayana kuwa, watafanya kila linalowezekana ndoto, matamanio na mahitaji waliyo nayo wananchi kwake yanatimia.
"Kazi ambayo tunapaswa kuifanya ni kuwasemea mambo mazuri ili kuongeza moyo na ari ya kufanya kazi zaidi". Amesema Alhaji Mwanga
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi )CCM) wilaya ya Mlele Wolfugan Mizengo Pinda amepongeza uamuzi uliofanywa na Mbunge wa Kavuu na kueleza kuwa, jambo hilo limejenga mhimili wa kuimarisha mahusiano baina ya wananchi wa madhehebu tofauti ya dini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Mwariko amesema, pale wanapopatikana viongozi wanaojitambua na kusimamia majukumu yao ipasavyo basi upo wajibu kwa wananchi kumshukuru Mungu, kuwafuata pamoja na kuwaombea kwa Mungu.
Akimuwakilisha Sheikh Mkuu wa mkoa wa Katavi, sheikh wa wilaya ya Tanganyika Sheikh Ayoub Mfutakamba amemshukuru Mhe, Pinda kwa kuwakutanisha pamoja wananchi wa Mpimbwe huku akimpongeza kazi nzuri anayoifanya katika wizara anayoiongoza hususan ile kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo katika mkoa wa Katavi.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amewataka wananchi wa Mpimbwe wilaya ya Mlele kuendelea kumuombea kwa Mungu wakati wa kutekeleza majukumu yake.
"Ni kazi kubwa sana kuongoza watu kwa sababu wewe huna maarifa yanayowazidi na wakati mwingine wao wana maarifa yanayokuzidi". Amesema Mhe, Pinda.
Amewataka waumini wa dini ya kiislamu na wananchi wa jimbo la Kavuu kwa ujumla kuwa karibu naye sambamba na kumtumia katika kuleta maendeleo ya jimbo kwa kuwa yeye yuko katika nafasi hiyo kama mwajiri wao.
"Msisubiri niharibikiwe kuweni karibu na mimi na msiponipa nafasi nitaona naenda vizuri wakati siyo". Alisema
Amewaambia wananchi wa jimbo la Kavuu kuwa, yeye kama mtumishi wao atawahudumia kwa haki na siyo hali zao kwa kuwa lengo lake ni kuhakikisha wale wenye haki wanapatiwa haki zao na siyo vinginevyo.
Aidha, ameongeza kuwa, katika kipindi cha cha uongozi katika jimbo la Kavuu atahakikisha Mpimbwe inafunguka katika maendeleo hivyo amewataka wananchi wa Mpimbwe kuungana ili kufungua milango yenye kheri.
Amesema hapendi uonevu katika maisha yake na kuweka bayana kuwa atawatumikia kwa haki na siyo kuangalia hali zao.
No comments:
Post a Comment