HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 25, 2024

Mvua zakwamisha wanafunzi wengi kwenda shule

Na Mwandishi Wetu

 

WANAFUNZI wengi leo katika Mkoa wa Dar es Salaam, wameshindwa kwenda shule kutokana na mvua inayoendelea kunyesha kuanzia usiku.

Mwandishi wa habari hizi amebaini hayo alipozungumza na walimu, wazazi na wanafunzi mbalimbali ambao wameeleza hali ya hewa imesababisha watoto wao wasiende shule.

Akizungumza na waandishi wa Habari jana mchana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda aliagiza katika kipindi hiki mvua zinavyoendelea  kunyesha, shule zinazoweza kuwapokea wanafunzi waliopata athari ya mvua zifanye hivyo ili waendelee na masomo.

Mkenda amesema hayo na kusisitiza kuwa taarifa nyingine za wanafunzi hao watakaopokelewa katika shule nyingine zitafuata baadaye katika maeneo watakayokuwa wamehamia.

“Kutokana na mvua nyingi zinazoendelea hapa nchini yapo maeneo mengi ambayo yamepata mafuriko na miundombinu ya elimu kuharibika kabisa. Maeneo kama Rufiji, Kibiti na baadhi ya maeneo mengine kutokana na athari hizo wanafunzi wameondolewa shuleni na zile shule kufungwa kwa sasa hivi.

“Kwa hiyo kama shule imefungwa katika eneo ambalo mafuriko yamezidi na maji yamejaa familia zimehama na kule walikohamia kama kuna usalama na kuna shule ipo karibu, zile shule ziwapokee wale wanafunzi halafu taarifa zao kutumia Maofisa Elimu Kata zitafutwe ziwekwe pale,

“Mbele ya safari tutajua wanafunzi kama watahama kwa kudumu kuhamia shule hizo au watapata tu elimu halafu baadaye watahamia shule nyingine,” amesema.

Amesema hilo litafanyika hata kwa shule binafsi ambazo zimeharibiwa na mvua kwa kumwagiza Kamishna wa Elimu kuwasiliana na wamiliki wa shule hizo.

Amesema serikali ipo tayari kusaidiana na wazazi ambao wanafunzi wao wapo katika shule binafsi ambazo zimeathirika kuwatafutia mahali pengine watakaposoma.

“Na kama mzazi anataka kumhamisha mtoto kwenye shule ambayo imeharibika kabisa tutaangalia taratibu na mwenye shule ile ili watoto waendelee kusoma kadri inavyowezekana, kwa hiyo shule za umma hata shule binafsi tungependa kwa kadri iwezekanavyo tuhakikisha kwamba shughuli za utoaji elimu hazikwami,” amesema.

Pia amesema Kamishna wa Elimu atatoa maelekezo kuwa ikionekana hali ya hewa si nzuri na ni hatari kwa watoto kutoka nyumbani kwenda shuleni, wazazi wana haki ya kuwaambia wasiende na shule husika ziangalie siku hizo zisihesabiwe katika siku za kufundisha ili kutafuta namna ya kufidia watoto kwenda shule.

Vile vile amesema walimu wakuu wanaweza kuangalia na kutathmini hali ilivyo ili kuzuia masomo kwa siku moja au mbili kulingana na hali ya hewa inavyoendelea.

“Walimu wakuu wafuatilie mpaka hapo hali itakapokuwa imetulia ili tuhakikisha kama kalenda imeenda vizuri muhimu tu ni kwamba kama ikitokea shule inabidi iache masomo kwa siku moja kwa sababu mvua ilikuwa nyingi sana au siku tatu lazima kutafuta mkakati wa kufidia ule muda ambao masomo hayakutolewa,” amesema.

Profesa Mkenda amesema kutokana na hali ilivyo hivi sasa, Kamishna wa Elimu atatoa mwongozo na kuruhusu  mabadiliko kidogo katika kalenda ya ufundishaji ili kama mvua zikizidi unapisha ili watoto wasiumie waweze kuendelea na masomo baadaye mvua zitakapokuwa zimetulia.

Amewataka waendeshaji wa magari ya wanafunzi kuchukue tahadhari kubwa ili kama kuna dalili zote za hatari wasiingize magari kwenye maji kwa sababu ili kuepusha hatari inayoweza kutokea.



No comments:

Post a Comment

Pages