HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 16, 2024

NCHI ZA AFRIKA ZAJIPANGA KUNUFAIKA NA KUNDI LA NCHI TAJIRI-G20


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za Afrika, waliojadili maeneo ya kipaumbele ambayo nchi za Afrika zinahitaji kuyasukumabkama agenda mahususi katika mikutano ya Kundi la nchi 20 Tajiri Duniani (G20) baada Umoja wa Africa kupewa kiti katika kundi hilo. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi za Kamisheni ya Umoja wa Afrika, kando ya mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Jijini Washington D.C, Marekani.

 

Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
 

TANZANIA imeishauri Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), kutumia kikamilifu fursa ya kiti cha uwakilishi wa Umoja wa Afrika katika Kundi la nchi Ishirini Tajiri Duniani (G20), kutetea maslahi ya nchi za Afrika ili ziweke kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokwaza maendeleo ya nchi hizo ikiwemo madeni makubwa, maradhi, kilimo kisicho na tija, mabadiliko ya tabia nchi, uharibifu wa mazingira  pamoja na matumizi hafifu ya teknolojia.

Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba,  wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za nchi za Afrika, uliofanyika  Kando ya Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), iliyoanza rasmi jana Jijini Washington D.C nchini Marekani.

Dkt. Mwamba alisema kuwa Tanzania inaona kuwa nafasi hiyo ni muhimu kwa kuwa itachangia kutimiza malengo yake pamoja na ya nchi za Afrika kutekeleza na kusimamia vipaumbele vyake vya kuimarisha uchumi na huduma za kijamii kwa wananchi.

Aliyataja maeneo manne ya kimkakati yanayotakiwa kupewa msukumo mkubwa katika G20, ikiwemo maendeleo endelevu ya kiuchumi, uhimilivu wa madeni na Sekta ya fedha, Ulinzi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi, Maendeleo ya kilimo, Usalama wa chakula, afya, biashara na uwekezaji.

Dkt. Mwamba alifafanua kuwa nchi za Afrika zinahitaji kusaidiwa kuwa na miundombinu ya kijani, nishati jadidifu, matumizi ya teknolojia za kidigiti vitakavyochochea ukuaji wa uchumi jumuishi utakaozinufaisha nchi zote za Bara la Afrika.

Aidha, alisema kuwa nchi Tajiri Duniani (G20), ziangalie uwezekano wa kuzifutia ama kuzipunguzia madeni nchi za Afrika ambazo nyingi, uchumi wake umeyumba kutokana na majanga mbalimbali ya kidunia ikiwemo Uviko 19, mizozo ya vita pamoja na mabadiliko ya Tabianchi ili kiasi cha fedha kinachopatikana ama kukusanywa ndani ya nchi hizo kiweze kitumika kuendeleza nchi zao badala ya kulipa madeni.
 
Dkt. Mwamba alishauri pia kuwa nchi za G20 zizizaidie nchi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa fedha na matumizi na kusaidia teknolojia zinazoweza kutumika kukabiliana na hali hiyo na kulinda kizazi cha sasa na cha baadae.

Akizungumzia kuhusu kilimo na Usalama wa chakula, Dkt. Mwamba aliushauri Umoja wa Afrika kuhakikisha kuwa Nchi za G20 zinawekeza katika uzalishaji na usalama wa chakula kwa kuongeza uzalishaji kupitia tafiti mbalimbali kwani kuwekeza katika chakula ndiyo maisha ya sasa na ya baadae ya nchi za Afrika.
 
Alisema kuwa ni muhimu nchi hizo zikazisaidia nchi za Afrika kuboresha miundombinu na kifumo yake yake ya afya na kukabiliana na majanga kupitia matumizi ya chanjo na matibabu ya uhakika na kuwaelimisha watoa huduma za afya. 
 
Aidha, Dkt. Mwamba alitoa wito kwa nchi Tajiri Duniani kuiona Afrika kama kitovu cha uwekezaji na biashara kwa kutumia masoko ya ndani na kufungua masoko kwenye nchi zao, kuwekezaji mitaji ya moja kwa moja kwenye sekta muhimu za kiuchumi kikiwemo, kilimo, utalii, viwanda na teknolojia.

Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, alisema kuwa hatua ya Umoja wa Afrika kupata uwakilishi katika Kundi la nchi Tajiri Duniani (G20) kutaimarisha sekta ya fedha na kuzitaka nchi hizo za Afrika kuwa na mipango ya ushirikiano ili kupeleka agenda zenye maslahi mapana ya nchi zao katika mikutano ya G20.

Alitolea mfano wa Kundi la Nchi Tajiri Duniani (G20) kuhakikisha kuwa fedha za kigeni zinapatikana kwa wingi ili kuimarisha utulivu wa salafu, pamoja na kupatikana kwa fedha za kuimarisha mazingira akieleza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi yanaziathiri nchi nyingi za Afrika.

No comments:

Post a Comment

Pages