Dar
es Salaam. Tarehe 6 Mei 2024: Benki ya CRDB imeandika historia nyingine
kwa kupokea cheti cha kimataifa cha masuala ya mazingira baada ya jengo
lake la Makao Makuu kukidhi vigezo vya kimataifa vya majengo yenye
kuzingatia uhifadhi wa mazingira.
Cheti hicho cha kwanza kutolewa kwa majengo ya hapa nchini, kinatolewa na taasisi ya International Finance Corporation (IFC) ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya Dunia chini ya programu yake ya EDGE (Excellence in Design for Greater Efficiencies).
Akikabidhi tuzo hiyo, Mkuu wa Idara ya Majengo Yanayolinda Mazingira wa IFC, Dennis Quansah amesema ulinzi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na ni muhimu kuangalia kila kitu kinachochangia uchafuzi wa mazingira yanayoleta mabadiliko ya tabianchi na athari nyingine kwa viumbe viishivyo duniani.
“Ni
furaha kwa IFC kulithibitisha jengo lenu kwamba linatunza mazingira.
Hili ni jengo la kwanza kwa Tanzania. Cheti hiki tunachowapa ni
utambulisho kwa taassisi na mashirika ya kimataifa yanayohamasisha
utunzaji wa mazingira. Matumizi ya maji, nishati na vifaa vya ujenzi ni
kati ya vigezo muhimu vinavyotumika kulitathmini jengo kabla ya
kulithibitisha,” amesema Quansah.
Mkuu
huyo amesisitiza kwamba Benki ya CRDB imeweka mfano unaopaswa kuigwa na
taasisi nyingine nchini ili kuyaboresha majengo yao na kuunga mkono
juhudi za kulinda mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya
kuishi.
Cheti
hicho ni uthibitisho wa juhudi za Benki ya CRDB sio tu yenyewe kulinda
mazingira bali kuwezesha juhudi zinazofanywa na watu wengine kupunguza
uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kufadhili miradi yenye mrengo wa kulinda
mazingira.
Sekta
ya makazi ni kati ya maeneo yanayochangia uchafuzi wa mazingira
kutokana na aina ya vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi wa nyumba,
matumizi ya maji pamoja na nishati.
Akipokea
tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela
amesema cheti hiki kinadhihirisha safari waliyoianza miaka mingi
iliyopita hata wakawa taasisi ya kwanza ya fedha ukanda wa kusini na
mashariki mwa Afrika kutambuliwa na Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa
Mataifa (GCF) Novemba 2019.
“Kwa
niaba ya menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya CRDB, ninafurahi
kupokea tuzo hii ya kulitambua jengo letu la makao makuu kwamba
linatunza mazingira tukikidhi vigezo kwenye vipengele vyote vitatu
vinavyozingatiwa na IFC kabla ya kutoa cheti.
Tumepunguza
matumizi ya nishati kwa asilimia 21 na matumizi ya maji kwa asilimia
27. Vifaa tulivyovitumia kwenye ujenzi navyo vinapunguza uzalishaji wa
hewa ya ukaa kwa asilimia 28 hivyo kutufanya kuwa juu ya kiwango cha
chini kinachokubalika,” amesema Nsekela.
Akifafanua
kuhusu vigezo hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Programu Endelevu wa Benki ya
CRDB, Ramla Msuya amesema katika jengo la Benki ya CRDB, taa huzima
zenyewe kama hakuna mtu ofisini na maji hayatoki iwapo hakuna mtu
anayetaka kuyatumia.
“Taa
zinatakiwa ziwake tu iwapo kuna mtu anahitaji mwanga na maji iwe
maliwatoni au jikoni, yatatoka iwapo yanahitajika. Huwezi kukuta maji
yanamwagika kwa kigezo kwamba mtu kasahau kufunga bomba, hapa kwetu
bomba linajifunga lenyewe kama hakuna anayelitumia, hizi ni sifa ambazo
hazipo kwenye majengo mengi nchini.
Vifaa
vilivyotumika kweny eujenzi wa jengo hili ambalo Rais Samia Suluhu
Hassan alilisifia wakati analizindua pia vinajali mazingira. Taka zote
zinazokusanywa humu ndani zinarejelezwa, huwezi kuon ataka zimezagaa
popote,” amefafanua Ramla.
Ili
kuziwezesha taasisi na watu wengine wanaotaka kuyaboresha majengo yao
yaendane na vigezo vya kimataifa vya kutunza mazingira, Nsekela amesema
Benki ya CRDB inatoa mikopo inayoendana na malengo hayo.
“Tunao
wabia zaidi ya 200 tunaoshirikiana nao kufanikisha uwezeshaji huu.
Benki ya CRDB peke yake inaweza kukopesha mpaka dola milioni 107 za
Marekani na ikishirikiana na GCF mkopo unafika dola milioni 250 na
hakuna kikomo tukishirikiana na wabia wetu wengine.
Tunafanya
hivi ili Tanzania nayo iwe miongoni mwa mataifa yenye miradi inayolinda
mazingira. Mwaka jana tulitoa Hatifungai ya Kijani na kukusanya fedha
nyingi kwa ajili ya miradi hii. Tunamkaribisha kila mwenye wazo au mradi
wa kulinda mazingira,” amesema Nsekela.
No comments:
Post a Comment