Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaabani akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, katika kikao kati ya Tanzania na Waziri wa Kodi wa Denmark, Mhe. Jeppe Bruus, kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jijini Nairobi nchini Kenya.
Na Ramadhani Kissimba na Farida Ramadhani, WF - Nairobi
Tanzania na Denmark zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika kutekeleza program ya maboresho ya mifumo ya kodi.
Hayo
yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis
Shaabani kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry
Mwamba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kodi wa Denmark,
Mhe. Jeppe Bruus, kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana
(Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), Jijini Nairobi nchini Kenya.
Alisema kuwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Denmark zimekubaliana
kuendelea kushirikiana katika kutekeleza program hiyo ambayo inasimamiwa
na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya Wizara ya Fedha.
“Tumekubalina
kuwakutanisha wataalam wa Tanzania na Denmark kupitia Ubalozi wao ili
kufanya tathmini na kuangalia maeneo yote muhimu yanayohitaji maboresho
katika kutekeleza program hiyo”, alisema Bi. Amina.
Bi. Amina
aliongeza kuwa kupitia wataalamu wa nchi hizo mbili (Tanzania na
Denmark), Serikali inatarajia maboresho yatakayofanywa katika program
hiyo yatayasaidia kuongeza ufanisi katika makusanyo ya mapato nchini.
Aidha
katika kikao hicho Denmark imeelezea maendeleo mbalimbali ya baadhi ya
masuala ambayo ilikubaliana na Tanzania kupitia ziara zilizofanywa na
Viongozi hivi karibuni.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa
Kodi wa Denmark, Mhe. Jeppe Bruus alisema Wizara ya Kodi nchini Denmark
itaendelea kutoa msaada wa kitaalamu kwa Serikali ya Tanzania katika
kuhakikisha inafanya maboresho ya program mbalimbali za kodi na
kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya nchi hizo mbili.
‘’Serikali
ya Denmark kupitia Wizara ya Kodi, inatambua umuhimu wa ushirikiano
uliopo kati ya nchi hizi mbili, hivyo ni muhimu kuendeleza ushirikiano
huo hasa kwa kusaidia katika eneo la utaalamu wa masuala ya kodi’’,
alisema Mhe. Bruus.
Aliongeza kuwa Denmark na Tanzania zina
historia ndefu katika masuala mbalimabli ya ushirikiano na kwa sasa nchi
hiyo mbali na kuendeleza ushirikiano katika masuala ya kodi, pia
inaangazia kukuza ushirikiano katika masuala ya kijamii na kiuchumi.
Katika
kikao hicho Waziri wa Kodi wa Denmark, Mhe. Jeppe Bruus alitumia fursa
hiyo kujitambulisha na kuelezea uwezo wa Wizara anayosimamia na kuitaka
Tanzania kufanya kazi kwa ushirikiano katika sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment