HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 11, 2024

Wazazi, walezi watakiwa kuchangamkia Junior Jumbo za CRDB Viwanja vya Sabasaba

MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

BENKI ya CRDB imeyatumia Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Tanzania, yanayoendelea kwenye Viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam, kuwahimiza wazazi na walezi kujitokeza kuwafungulia watoto wao Akaunti za Junior Jumbo, zinazoweza kutumika kulipia bili mbalimbali za mtoto - kielimu na kiafya.

 Junior Jumbo ni akaunti isiyo na makato ya mwezi inayofunguliwa kwa Sh. 20,000 ambayo licha ya kumjengea mtoto utamaduni chanya wa kujiwekea akiba maishani, ina ukomo wa kutoa pesa bila makato ili kuchochea uwekaji akiba, iwapo mzazi ama mlezi atatoa mara nne zinazoruhusiwa kwa mwaka.

Wito huo umetolewa na Afisa wa Benki ya CRDB Tawi la Temeke, Doreen Hermes, alipozungumza na wanahabari katika banda la benki hiyo kwenye viwanja hivyo, akisisitiza Junior Jumbo ni akaunti rafiki kwa ustawi wa maisha ya sasa na baadaye ya mtoto, ambayo anapewa uhuru wa kuitumia anapofikisha miaka 18.

“Banda letu la CRDB lililopo hapa Sabasaba na matawi yetu kote nchini, yanaendelea na utoaji wa huduma mbalimbali na masuluhishi ya kipesa, ikiwemo ufunguzi wa akaunti zote. Wito wetu ni kwa wazazi na walezi kujitokeza hapa kufungua Junior Jumbo Account kwa ajili ya watoto wao.

“Hii ni akaunti maalum kwa ajili ya matumizi yanayomuhusu mtoto kwa sasa na hata maisha yake ya baadaye. Ni akaunti isiyo na makato, ambapo mzazi anapaswa kuja kufungua akiwa na picha mbili za ‘passport size’ za mtoto, cheti cha kuzaliwa cha mtoto, kitambulisho cha mzazi na kianzio cha shilingi 20,000.

“Kupitia akaunti hii, mzazi ama mlezi ataweza kulipia bili za mtoto, ada na michango mbalimbali ya shule, malipo ya huduma za hospitali kwa mtoto na mengineyo mengi, kulingana na kiasi alichomuwekea mtoto husika katika akaunti yake,” alibainisha Doreen.

Aidha, Afisa huyo alisema mwitikio wa wananchi katika banda la lililpo Viwanja vya Sabasaba ni mkubwa sana, huku akiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi zaidi kutembelea tawi lao katika siku chache zilizosalia kuelekea kufunga kwa maonesho hayo, ili kujipatia huduma mbalimbali tawini hapo.


 

No comments:

Post a Comment

Pages