NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WIKI mbili tangu Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), kutoa taarifa za kukamatwa kwa wanafunzi feki 17 waliokuwa wakijaribu kuwafanyia mitihani wanafunzi wa chuo hicho, Serikali imejiapiza kuwabana na kuwakomesha ili kulinda mfumo wa elimu nchini, na kwamba bado vyuo vikuu nchini viko salama na vinazingatia maadili.
Juni 28 mwaka huu, OUT kupitia Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda, kilisema wanafunzi feki 17 walikamatwa katika vituo vya mitihani vya Kinondoni na Ilala, wakijaribu kuwafanyia wanafunzi wa chuo hicho mitihani hiyo iliyoanza Juni 3 hadi 24, ikihusisha vitu 53 vyenye wanafunzi 10,417.
Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya mkutano wake na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema Serikali inapambana kukomesha, kwani vyuo vikuu vinazingatia maadili na weledi ili kuhakikisha vinazalisha wahitimu wenye sifa.
“Suala la udanganyifu na majaribio ya udanganyifu kwenye mitihani lipo dunia nzima, suala kubwa ni juhudi gani zinafanyika kudhibiti vitendo hivyo. Kwahiyo pamoja kwamba tunajua kuwa tunaendelea vizuri na udhibiti wa matukio hayo, upo msemo usemao; adhaniaye amesimama, aangalie asianguke.
“Kila tunaposikia ama kushuhudia tuhuma hizi za udanganyifu, tunaumizwa nazo sana. Imekuwa hivyo katika ngazi mbalimbali kuanzia mitihani ya kidato cha nne, cha sita na vyuo vya kati na vyuo vikuu na tumekuwa tukichukua hatua kali ambazo kwa bahati mbaya zinawaumiza hata baadhi ya wawekezaji wa sekta ya elimu.
“Tunasimama imara katika kukomesha vitendo hivi, kwa sababu tunatambua madhara ya udanganyifu kwenye mitihani ni makubwa sana, kwamza linaondoa usawa miongoni mwa wanafunzi, ambao kimsingi wanatakiwa kupimwa kwa haki, asiwepo wa kupita kwa udanganyifu pasipo na juhudi zake,” alisemma Profesa Mkenda.
Akitolea mfano udaktari, Profesa Mkenda alisema ni hatari kubwa kuwatumia madaktari waliofaulu kwa kutumia udanganyifu na kwamba athari zake zinaenda kuumiza wasiohusika na mchakato huo, ambao ni wagonjwa watakaopitia mikononi mwa madaktari hao wasio na sifa kielimu.
“Udanganyifu katika ngazi yoyote ile ya elimu, ni saw ana kulea ama kufumbia macho rushwa klwa wanafunzi wetu, kwamba wewe mwanafunzi njia nzuri na rahisi ya kufanikiwa ni kufanya udanganyifu, mbaya zaidi hatua kali tunazochukua, baadhi ya watu wanatulaumu kwamba tumekuwa wakali sana.
“Tunaomba watuelewe, kwani tunafanya hivyo kwa sababu tunapenda kuulinda mfumo wetu wa elimu, ndio maana Baraza la Mitihani la Taifa limesimama kidete na sasa limekuja na sheria kali ili kuwabana zaidi wadanganyifu na kama mlivyosikia juzi hapa wamehukumiwa, tunazishukuru mamlaka,” alisisitiza Prof. Mkenda.
Kuhusu vyuo vikuu, Prof. Mkenda alisema vyote vina kanuni zake za kusimamia mitihani yao ambazo zinafahamika na TCU inazifahamu, ikiwemo kufukuzwa chuo moja kwa moja kwa wanafunzi wanaokamatwa kwa udanganyifu, ambapo aliviomba vyuo viendelee na adhabu hizo bila kusita.
Aidha, Profesa Mkenda aliviomba vyombo mbalimbali vya habari nchini, kutoa ushirikiano kwa Serikali kupitia Baraza la Mitihani, Tume ya Vyuo Vikuu na vyombo vya dola kwa kutaja viashria na wahusika wa vitendo vya udanganyifu wa mitihani kwa wanafunzi, badala ya kuficha majina na kuandika magazetini kila siku.
No comments:
Post a Comment