Afisa Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Richard Mosile akitoa elimu ya Mazingira kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma walipotembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, Agosti 4,2024.
Afisa Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Raphael Maziku akitoa elimu ya Muungano kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Chinangali, Dodoma wakati walipotembelea Banda la Ofisi hiyo katika Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma Agosti 2,2024.
Maafisa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwa katika picha ya kumbukumbu na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chinangali mbele ya banda la Ofisi ya Makamu wa Rais mbele ya Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais mara baada ya kupata elimu ya Muungano, katika Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane mkoani Dodoma yanayofanyika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni, Agosti 2,2024. (NA MPIGAPICHA WETU).
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya) Mhe. Dkt. Festo Dugange amekishauri Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni (NCMC) kupanua wigo wa utoaji wa elimu kuhusu fursa na manufaa ya biashara hiyo kwa wananchi.
Dkt. Dugange amesema hayo (Agosti 4, 2024) wakati alipotembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa iwapo elimu ya kutosha kuhusu biashara ya kaboni itatolewa kwa wananchi hususani kupitia fursa ya upandaji miti itasaidia uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na kuongeza kipato katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.
Dkt. Dugange amesema zipo baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatekeleza miradi ya biashara ya kaboni na hivyo kutoa ushauri kwa Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni (NCMC) kubuni na kuweka mipango mahsusi ya kushirikiana na Halmashauri hizo katika utoaji wa elimu.
“Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) hakina budi kujitangaza ili kiweze kufahamika na kufikia wadau wengi ikiwezekana hata kufungua ofisi za Kanda katika Mikoa mbalimbali nchini.
Amesema ni wakati mwafaka kwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu ya biashara ya kaboni inatolewa kwani bado jamii haina hawana uelewa wa kutosha kuhusu kaboni pamoja na fursa na faida zilizopo katika biashara hiyo.
Naibu Waziri Dugange pia aliitaka Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia NCMC kufanya mikutano na makongamano na wadau ili kutoa elimu kwa ikiwemo wananchi na taasisi mbalimbali za uwekezaji ambao ndio walengwa wakubwa wa biashara ya kaboni nchini.
Amesisitiza kwa kuwepo kwa wataalam wengi ambao watasaidia katika kutoa elimu hiyo ila kwa sasa inaonekana bado kuna uhaba wa wataalamu kwenye eneo hilo lakini jitihada ikiongezeka basi matunda yake yataonekana kwa kila mmoja.
Aidha Dkt. Dugange amezitaka Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira na kuhakikisha miti yote inayopandwa inatunzwa na kustawi.
Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yaliyoanza tarehe 1-8 Agosti, 2024 katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma yakiwa na kauli mbiu isemayo Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
No comments:
Post a Comment