Semina hiyo ya wakaguzi na maofisa wanaosimamia dawati la jinsia katika vituo na wilaya za kipolisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Dar es Salaam ikiendelea. |
MWANDISHI WETU
MABOSI wengi katika mazingira ya kazi hupenda kuomba rushwa ya ngono kwa wanawake wanaonyonyesha ili nao wanyonye maziwa ya mama, bila kujali kuwa kufanya hivyo, wanawadhulumu watoto wachanga; Amebainisha Dk Christina Onyango wa Jeshi la Polisi.
Amebainisha hayo wakati akitoa mada kwa wakaguzi na maofisa wanaosimamia dawati la jinsia katika vituo na wilaya za kipolisi katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Dar es Salaam.
Amesema hayo katika siku ya kwanza ya mafunzo iliyohusisha askari polisi wa vyeo vya chini kujengeana uwezo kuhusu namna ya kutekeleza kampeni ya Jeshi la Polisi isemayo: “Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa.”
Kampeni hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi wapya uelewa na uwezo wa kubaini viashiria vya ukatili wa kijinsia na makosa mengine wawapo katika mazingira mapya ya kidato cha kwanza, tano au mwaka wa kwanza vyuoni.
Kwa nyakati mbalimbali tangu mwanzoni mwa mafunzo hayo, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Leah Mbunda; Mkuu wa Dawati hilo katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Glory Urassa na Mratibu wa Mafunzo hayo, Mkaguzi wa Polisi, Dk Christina wamesema lengo lingine kubwa la kampeni hiyo ni kutahadharisha wanafunzi na wanachuo wapya dhidi ya tabia potofu wanazokutana nazo waingiapo shuleni na vyuoni.
Kuhusu tabia chafu ya baadhi ya wanaume wenye madaraka, Dk Christina amesema; “Wanaume wengine wakiwamo wenye mamlaka wanapenda kunyonya maziwa ya wanawake wanaonyonyesha.”
“Sasa hao wenye mamlaka kazini mjamzito akijifungua na kwenda kutaka ruhusa kwa ajili ya kwenda kunyonyesha mtoto, baadhi wanatumia nafasi hiyo kumkandamiza mwanamke huyo kwa kudai riushwa ya ngono…” amesema Christina.
Akaongeza: “Wanatumia fursa hiyo ili wawe wananyonya maziwa ya mama huyo huku wakijua kuwa wanamdhulumu mtoto haki yake ya kupata chakula”.
Imebainika kuwa, wanaume wengi wanaopenda kunyonya maziwa ya wanawake wanaonyesha hufanya hivyo wakiamini kuwa, maziwa hayo yana nguvu ya kukata uchovu wao unaotokana na ulevi wa pombe.
Ofisa wa Polisi Jamii katika Wilaya ya Kipolisi ya Kati katika Mkoa wa Ilala, Rose Mbaga alitaka wanawake waelimishwe ili wasimalize nguvu zao kwa kuhanagaikia madeni mbalimbali wanayokopa huku mengi yakiwa ne kutojulikana yamesaidia vipi familia badala yake, wawe na yanashughulikia malezi ya watoto katika familia na jamii zao.
“Wanawake tusijisahau na kumaliza nguvu zetu zote kwenye vikoba. Unakuta mwanamke mmoja ana vikoba karibu 20 sasa hatulii; hana muda wa kuhudumia watoto wala mume wake ndio maana ninasema tutafute midahalo na akina mama tuwafuate katika maeneo yao hata ya kibiashara huko huko tusungumze nao…” amesema Rose.
Mafunzo hayo kwa askari, wakaguzi na maofisa yamelenga kuwafanya washiriki kuwa na uelewa sahihi, wa pamoja na wa kutosha katika kampeni hiyo kuhusu ukatili wa kijinsia ukiwamo wa rushwa ya ngono.
“Kwetu kampeni ya Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa inawalenga wanafunzi wapya wanaoanza masomo yao katika ngazi za kidato cha kwanza, kidato cha tano, vyuo vya kati na vyuo vikuu katika eneo letu la Mkoa wa Kipolisi wa Ilala,” amesema Christina.
“Miongoni mwa mada na mambo yatakayohimizwa katika kampeni hiyo kwa wanafunzi,” Dk Onyango anasema ni pamoja na uzalendo, tunu za taifa pamoja na maana, madhara na namna ya kuepuka ukatili wa kijinsia mtandaoni na rushwa ya ngono.
Dk Christina amesema: “Katika kampeni hii tunayoanza mwezi huu na kuhitimishwa Februari mwakani baada ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kuripoti shuleni, mada kuhusu rushwa ya ngono itatiliwa mkazo zaidi kwa wanafunzi wa vyuo vya kati na vyuo vikuu wawapo vyuoni kwao.”
No comments:
Post a Comment