HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 08, 2024

MZIRAY AKOSHWA NA WALENGWA TASAF

Na Mwandishi Wetu

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), umewezesha walengwa wa mfuko huo kutumia ruzuku wanayopata kushiriki kilimo, hali ambayo imekuwa ikiwaongezea kipato na kuwa na uhakika wa chakula.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shadrack Mziray wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane ya Kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya Nzunguni mkoani Dodoma.

Mkurugenzi huyo amesema uamuzi wa walengwa  kutumia rukuzu ambayo wanapewa na TASAF kwenye kilimo imemfurahisha na kuahidi kuwa watahakikisha wanawatafutia masoko ili waweze kuuza bwa bei nzuri.

Mziray amesema TASAF imekuwa ikitoa ruzuku kwa viwango tofauti kulingana na sifa ya mlengwa, hivyo kitendo cha baadhi yao kuitumia kwenye kilimo ni cha kupongezwa na kuungwa mkono.

Amesema dhamira yake ni kuona asilimia 26 ya Watanzania maskini inapungua hivyo kuwataka wanufaika wengine kubuni vyanzo vya mapato, ili waweze kupata maendeleo na kuondoka kwenye umaskini.

Amesema wapo walengwa kutoka wilayani Bahi mkoani Dodoma ambao wameonesha mfano kwa kulima zao la mpunga, ila kutokana na kuimarika kiuchumi wameamua kusubiri bei ipande ndio wauze, jambo ambalo limeonesha TASAF imeleta mabadiliko changa.

“Wananchi tunaowapa ruzuku wengi wao wanajihusisha na shughuli za kilimo, kwa kugawanya kiasi cha ruzuku na kutumia kwenye kilimo kwa kununua pembejeo, hivyo kusema kweli TASAF imesaidia sekta ya kilimo kwa asilimia kubwa.

Kule mkoani Njombe kupitia Mkuu wa Mkoa Anthony Mtaka amefanya ubunifu kwa kushirikiana na Mpango wa Kukuza Kilimo Kanda ya Kusini (SAGCOT), wameweza kuwapatia walengwa wa TASAF miche10 bora ya parachichi, tuliwatembelea baadhi yao na walengwa wameambiwa baada ya miaka mitatu watakuwa wametoka kwenye umaskini,” amesema

Mziray amesema TASAF inaangalia namna ya kuungana na taasisi zingine zilizopo kwenye halmashauri, pamoja na Shirika la Viwanda Vidogo, Vidogo (SIDO) ili kuhakikisha bidhaa za walengwa zinakuwa bora na kuingia katika soko la ushindani.

Amesema pia wanahakikisha walengwa wanatengeneza bidhaa ambazo zimefanyiwa utafiti ili kuhakikisha zinapata soko bila shida.

Kwa upande wake Beno Mgaya, Mwenyekiti wa  Lisitu Agri Bussines chini ya mwavuli wa SAGCOT alisema wanachokifanya ni kuwaondoa walengwa katika mtazamo hasi kuwa wao ni maskini  wakati wanamiliki mali nyingi ikiwemo ardhi ya kilimo.

Mgaya amesema kwa kushirikiana na TASAF wamefikia zaidi ya walengwa 4,780 kutoka katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Morogoro, Mbeya, Dodoma na kwingine ambao kwa sasa wanashiriki kwenye kilimo.

“Kwa kushirikiana na TASAF tumewafanya walengwa kuingia katika kilimo biashara, hivyo kila mlengwa anaweza kulima mazao kama parachichi, viazi mviringo na mengine na miaka mitatu ijayo wataondoka kwenye umaskini,” amesema.

Naye Mlengwa Mlanja Magesa mkazi wa kijiji cha Mapilinga Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza, amesema TASAF imekuwa neema kwake kwani ameweza kusomesha watoto wake wanne bila shida.

“Nina mtoto anamaliza darasa la saba Shule ya Msingi Mapilinga mwaka huu, wengine watatu wapo Shule ya Sekondari Igokelo. Kipindi naingia TASAF nilikuwa nimepanga ila nimejenga naishi kwangu.

Lakini pia nimepata ujuzi wa kutengeneza bidhaa kama sabuni ya mche, maji na nyingine nyingi ambazo zinatumika kuoshea vyombo na vyoo,” amesema.

Magesa ambaye anapokea shilingi 31, 000 kwa mwezi alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kuipatia TASAF fedha ili iweze kusaidia wananchi maskini.

Shafii Hamad Faki kutoka Mgogoni Wilaya ya Wete Kisiwani Pemba, amesema TASAF imechangia mabadiliko makubwa kwenye maisha yake, ikiwemo kupata mlo kamili na kusomesha watoto wake.

“Tangu 2015 nipo TASAF ambapo nimenufaika kwa ujuzi, kwani kwa sasa najua kutengeneza sabuni, mafuta ya kuchua, tunafuga nyuki na pia kuna vikundi vya kijasiriamali,” amesema.

Faki amesema TASAF imenufaisha kijiji chake kwa kujengewa shule ya sekondari, kupata maji kutoka umbali wa kilomita tano na mengine mengi.
 

No comments:

Post a Comment

Pages