HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 06, 2024

Pembejeo za asili zavutia wakulima nchini

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

 
MATUMIZI ya pembejeo za asili kama mbegu, viuatilifu na mbolea kwenye kilimo zimedaiwa kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wanaolima kwa njia ya kilimo ikolojia hai.

 
Hayo yamesemwa jana na wadau mbalimbali wa kilimo ikolojia hai wanaoshiriki maonesho ya kitaifa ya Nanenane yanafoyanyika mkoani Dodoma.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Ofisa kutoka Taasisi ya Alliance Generies ya mkoani Simiyu, Masalu Samweli alisema wao wanajihusha na kilimo ikolojia hai kwenye zao la pamba takribani miaka mitatu na matokeo yamekuwa mazuri.

Masalu alisema wakati wanapeleka elimu ya kilimo ikolojia hai walikuta wakulima 1,000 wa pamba Mkoa wa Simiyu ila hadi sasa wamefikia wakulima zaidi 22,000, huku mikoa mingine ikianza kilimo hicho kwa kuwa wenzao wamekuwa wakifaidika zaidi.

Alisema Alliance Generies ilipofika ilianza kutoa elimu kuhusu faida za kilimo ikolojia hai kiafya, kimazingira na utunzaji wa ardhi, jambo ambalo limepokelewa vizuri.

“Kwa uzoefu wangu wa miaka mitatu ya kutoa elimu kuhusu kilimo ikilojia hai, uzalishaji wa mazao yasiyo na kemikali, hivyo wameweza kuona faida, hasa kupunguza gharama za uzalishaji, wameweza kutunza afya na uhakika wa masoko,” alisema.

Masalu alisema pia Alliance Gineries imeweza kuongeza bei ya pamba ambayo inazalishwa kwa njia ya kilimo ikolojia hai, hali ambayo imekuwa kivutio kwa wakulima wa zao hilo katika mikoa mbalimbali, kama Mwanza, Geita, Shinyanga, Tabora na Mara.

Ofisa huyo alisema pia kampuni hiyo imeweza wakulima kupata dawa za molasesi kutega mitego na kupanda mazao ambayo yanazuia wadudu kushambulia pamba.

“Wakati tunaingia kwenye zao la pamba wakulima walikuwa wanapata kilo 200 kwenye hekari moja, ila kilimo ikolojia hai kimeongeza mavuno hadi kufikia tani moja kwa hekari. Hivyo bei ya zao hilo kwao inaongezeka kulingana na soko hilo duniani,” alisema.

Kwa upande wake  Mkulima wa zao la Pamba wilayani Ikungi mkoani Singida, Solo Lameck alisema tangu kuanza kulima kwa mbinu za kilimo ikojojia hai ameweza kunufaika, hivyo kuitaka jamii kujikita huko.

“Kilimo hiki kinapunguza gharama kwa mkulima, hasa kwenye pembejeo, kama vile matumizi ya pumba za mbao na pamba yenyewe. Lakini pia tumekuwa tukizingatia vipimo kwenye kilimo,” alisema.

Lameck alisema katika zao la pamba ambalo wanalima kwa njia ya kilimo ikolojia hai wanatumia kipimo cha sentimita 30/30 shina hadi shina na 60/60 mstari hadi mstari kimekuwa na matokeo kwa mkulima zaidi.

Alisema elimu ya kilimo ikolojia hai mkoani Singida imeweza kuongeza wazalishaji wa zao la pamba na wameweza kubadilika kiuchumi na kiafya.

Naye Ofisa Masoko wa Kampuni ya Safari Organic, Cosmas Mpobozi amewataka wakulima kutumia mbolea asili kwani imeonesha kuwa na virutubisho muhimu kwa mazao, ardhi na mazingira.

Felician Puis kutoka Shamba la Kilimo Ikilojia Hai SJS Kwa Nyange wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro alisema katika shamba hilo wana miradi zaidi 45 ambayo inazalishwa kwa kwa njia asili, hivyo kuwataka wakulima kwenda kujifunza.

Pius alisema pia wanazalisha virutubisho na viuatilifu vya mimea kwa kutumia rasilinali zinazowazunguka wakulima, ikiwemo msitu wa mbogamboga.

“Katika shamba letu tumetumia vimelea rafiki vya shambani ambavyo vinadhibiti harufu mbaya inayopatikana kwenye mazizi ya mifugo kama nguruwe,” alisema.

Mtaalam huyo alisema pia SJS inagundua zao la dragoni ambalo linakubali kuota katika maeneo mbalimbali na soko lake ni la uhakika.

Akizungumzia teknolojia hizo za kilimo ikilojia hai Mtafiti kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) alisema kupitia Shamba la SJS ameweza kujifunza mbinu za asili za kudhibiti magonjwa kwenye mimea na anaomba wakulima kurejea katika mbinu hizo.

“Nipo Chuo Kikuu cha Nelson Mandela ambapo nasoma Shahada ya Uzamivu (Phd) ya Ugonjwa wa Mimea, ila kwa sasa nipo SJS kujifunza mbinu zinazotumia kudhibiti wadudu kusema kweli nimeona matokeo chanya, hivyo napenda kuwaomba wakulima wajikite katika kilimo hicho kwani hakina sumu,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages