HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 13, 2024

TPA YATOA MILIONI 260 HOSPITALI YA TEMEKE

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari  Tanzania (TPA) imetoa zaidi ya Sh. milioni 260 kwa ajili ya maboresho na ukarabati wa jengo la usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam.

Kati ya kiasi hicho cha fedha, TPA imetoa milioni 251 kugharamia ukarabati wa jengo la wagonjwa na milioni 10 nyingine zilitumika kununua  viti mwendo 20 na vifaa tiba vingine kwa ajili ya hospitali hiyo,

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa kupokea msaada huo kwa niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Mkuu wa Wilaya ya Temeke (DC) Sixtus Mapunda aliishukuru TPA kwa msaada huo na kusema TPA inajali jamii na kuziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo.

‘’Kipekee niipongeze Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam kwa kujitolea ukarabati wa jengo hili kwa ajili ya huduma ya usafishaji wa damu hapa hospitali ya Temeke.

Ukarabati huu utasaidia kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji’’ amesema DC Mapunda.

Amesema kuwa Serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza vya kutosha katika sekta ya afya hapa nchini, lakini pia bado inahitaji na kuthamini michango mbalimbali ya wadau wakiwemo TPA katika kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba.

Amesema uboreshaji wa huduma za afya ni moja ya vipaumbele vikubwa vya Rais Samia, hivyo kwa kiasi kikubwa TPA wanaunga mkono jitihada hizo.

“Tunawashukuru sana TPA katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia za kuboresha sekta ya afya hapa nchini inayogusa maisha ya watu.

Uboreshaji wa sekta ya afya unasaidia watu kuwa na afya njema na kushiriki  kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi yetu,” amesema.

Akitoa maelezo ya utendaji wa hospitali hiyo, DC Mapunda amesema kuwa uhitaji wa watu wanaohitaji huduma ni mkubwa ambapo kwa mwaka 2022/2023, Hospitali ya Temeke ilihudumia wagonjwa 9,566 kwa watu waliokuwa na magonjwa yasiyoambukiza, ikilinganishwa na mwaka 2023/2024, ambapo  wagonjwa 11,175 walihudumiwa, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 14.4.

Amesema kuwa vyanzo vya magonjwa hayo yasiyoambukiza ni pamoja na ulaji usiofaa, ikiwemo matumizi ya chumvi na sukari kupita kiasi, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na kutofanya mazoezi.

“Katika kukabiliana na magonjwa hayo, amesema kuwa  serikali imejipanga pamoja na mambo mengine, kuongeza kasi ya elimu na uhamasishaji wa jamii katika kuzuia na kudhibiti magonjwa hayo na kuijengea mazoea ya kufanya  uchunguzi wa matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza na kufanya mazoezi,” amesema.

Hata hivyo, DC Mapunda amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya ina mpango wa kuziwezesha hospitali zote za rufaa za mikoa kutoa huduma ya kusafisha damu ili kutoa huduma kwa wananchi karibu zaidi na maeneo yao.

Akizungumzia juu ya msaada huo, Meneja wa Mizigo Mchanganyiko wa bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus amesema wameguswa na mahitaji hayo muhimu ya hospitali hiyo na kuamua kutoa kiasi hicho cha pesa katika kuunga mkono jitihada za Serikali.

“Mwaka jana mwezi Aprili, tulitoa msaada wa viti mwendo (wheelchairs) hopsitalini hapa, ndipo uongozi ulituomba msaada wa ujenzi wa jengo la usafishaji wa damu na sisi kama wadau bila kusita tukatoa kiasi hicho cha fedha ili kazi iendelee kama kauli mbiu ya Rais Samia inavyosema,” amesema.

Akiongelea juu ya msaada huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dk Joseph Kimaro ameipongeza TPA kwa mchango wao ambao utagusa maisha ya watu wengi .

Dk Kimaro amesema kuwa waliamua kujenga jengo hilo kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya wagonjwa wa figo ambapo 2023 kulikuwa na wagonjwa 412, hivyo ikapelekea kuanza mchakato wa ujenzi wa jengo hilo na sasa kwa jitihada za TPA limekamilika.



No comments:

Post a Comment

Pages