HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 05, 2024

WAKULIMA WAUNGA MKONO KAMPENI YA MBEGU NI UHAI

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

 

WAKULIMA wanaotumia mfumo wa kilimo ikolojia hai nchini, wameunga mkono Kampeni ya Mbegu ni Uhai inayofanywa na Mtandao wa Uhuru wa Chakula Afrika (AFSA), wakidai inaenda kuleta mapnduzi katika sekta hiyo.

Wakulima hao wametoa kauli ya kuunga mkono  wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hii, kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa mkoani Dodoma.

Mkulima kutoka Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Morogoro (MVIWAMORO), Rehema Kisimikwe amesema yeye ni mnufaika wa kilimo ikolojia hai, hivyo anaunga mkono kampeni ya mbegu ni uhai kwa kuwa inafaida nyingi kwao.

Rehema amesema mbegu asili zinapunguza gharama kwa mkulima tofauti na mbegu za viwandani, hivyo kuwashauri wakulima kuzitumia.

“Kilimo ikolojia, tunalima kwa majembe ya mkono, tunatumia mbolea za asili kama mwarubaini,  zinastahimili ukame, hazisumbuliwi na wadudu, hazitumii kemikali kutunza, mazao yana ladha, safi na salama,” amesema.

Amesema kilimo ikolojia kimemuwezesha kusomesha watoto hadi vyuoni, mmoja akisoma Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na mwingine Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kujenga nyumba na kumudu mahitaji ya familia.

“Nalima mahindi, mtama na mbaazi kwa njia ya kilimo ikolojia nimepata mavuno mengi, pamoja na kuboresha afya,” amesema.

Naye Foime Daniel wa kijiji cha Manchari A Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma amesema  mbegu asili zimefanya mageuzi makubwa kwenye maisha yake.

Foime amesema kwa sasa anamiliki zaidi ya heka 15 za mazao ya mahindi, mtama, alizeti, njugu na karanga.

“Mimi nimepiga hatua kubwa tangu kukutana na Mtandao wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), kwani nimefanikiwa kujenga, nimenunua mifugo na kununua mashine ya kupukuchua alizeti. Kubwa zaidi ni ninapata mavuno mengi ambapo hekari moja naweza kuvuna gudia 20 kutoka nane za awali,” amesema.

Miza Chiwanga kutoka Mtaa wa Chololo  mkoani Dodoma amesema matumizi ya mbegu asili yameleta mapinduzi makubwa katika maisha yake, ikiwemo kujenga nyumba na kusomesha watoto.

Miza amesema ni wakati muafaka kwa serikali kuweka mkazo katika matumizi ya mbegu asili kwa kuwa zinahakikishia walaji uhai.

Kwa upande wake Renalda Bayo Mkulima kutoka Kikundi cha Jitegemee Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Arusha (MVIWARUSHA), amesema matumizi ya mbegu asili yataifanya jamii kuwa salama kiafya.

“Matumizi ya mbegu na mbolea asili kwenye kilimo yanatengeneza kizazi bora na salama cha kesho, ila hizi zenye kemikali ni hatari kwa afya ya walaji na ardhi,” amesema.

Mkulima Juma Mbwambo kutoka Wilaya ya Muheza amesema kilimo ikolojia hai kimemfanya aishi maisha bora. Kwa kuongeza kipato na afya bora.

Naye Matrida Mwambe kutoka Masasi mkoani Mtwara amesema kilimo ikolojia hai ni uhakika wa soko la ndani na nje, hivyo kuwataka wakulima kujikita katika huko.

“Mimi na wenzangu tisa tunalima mbaazi, ufuta na mahindi kwa njia ya kilimo ikolojia hai, baada ya kupatiwa elimu na SwissAid, kusema kweli tumeimarika kiuchumi,” amesema.

Pelagia Gaudance kutoka Karatu amesema mwaka 2018 alikutana na Shirika la IDP ambalo lilimpatia elimu ya kilimo ikolojia hai na leo anajivunia mafanikio.

Amesema yeye anajihusisha na kilimo ikolojia hai  cha mahindi, maharage, mbaazi, alizeti na matunda mbalimbali.

Kwa upande wake Tatu Magongo wa Kikundi cha Muungano kijiji cha Muhenda, wilayani Kilosa amesema mbegu za asili zinapaswa kuungwa mkono kwa kuwa kina matokeo chanya.

“Mazao yanatokana na mbegu asili yanakuwa salama na bora kwa mlaji, ila pia mavuno ni mengi ambapo kwa sasa heka moja napata gunia 20, mahindi 20 hadi 25 kutoka gunia sita za awali,” amesema.

Amesema kilimo hicho kina ni ufumbuzi wa magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na mengine.

Agustino Joseph kutoka Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji mkoa wa Manyara (MVIWAMA), amesema mbegu za asili ni tunu na zina lishe bora kwa mlaji,

“Serikali inapaswa kutambua mbegu za asili ni salama kwa ajili ya kizazi hiki na kijacho, ujumbe wa AFSA kuwa Mbegu ni Uhai hauna shaka kabisa, kwani sisi tunaolima tunaona,” amesema.

Wawakilishi wa mashirika yanayohamasisha kilimo ikolojia hai yakiwemo, Mtandao wa Baionuai Tanzania (TABIO), SwissAid, TOAM, We Effect, SJS Organic, McDonald Organic, Inades Formation, Consenut, Floresta, IDP na Kilimanjaro Permaculture Community (KPC).

Kijani Hai, Farm Redio International, Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Shirikisho la Wakulima Tanzania (SHIWAKUTA), Pelum-Tanzania, Kijani Hai, Agroecology Hub Tanzania, Biovision Africa Trust, Safari Organic Fertilizer Mtandao wa Uhuru wa Chakula Afrika (AFSA) na Vi Agroforest wamesitiza umuhimu wa matumizi ya mbegu asili kama njia ya  kuwa na jamii yenye afya bora.



No comments:

Post a Comment

Pages