HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 12, 2025

TARURA Bagamoyo Yaendelea Kuweka Taa za Barabarani

Na Miraji Msala, Bagamoyo – Pwani


Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Bagamoyo umeendelea kuboresha miundombinu ya mwangaza kwa kuweka taa za barabarani katika mitaa mbalimbali ya wilaya hiyo, hatua inayolenga kuongeza usalama na kuimarisha shughuli za kiuchumi hasa nyakati za usiku.


Mhandisi wa TARURA Bagamoyo, Mbaraka Msiseme, amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023, ofisi yake ilipokea shilingi milioni 500 ambazo zilitumika kufunga taa 170 katika maeneo tofauti ya mji na vijiji vya Bagamoyo.

Tumeweka taa katika mitaa mbalimbali ili kuboresha mwanga na usalama wa watumiaji wa barabara. Hivi sasa wananchi wanafanya shughuli zao hadi usiku bila hofu, jambo ambalo limeongeza uhai wa mji,” alisema Mhandisi Msiseme.


Ameongeza kuwa TARURA ipo katika maandalizi ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo mpango ni kuongeza taa nyingine 100, ili kufikia maeneo zaidi ambayo bado hayajafikiwa.


Aidha, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya mwangaza, akisema hatua hiyo imekuwa kichocheo cha maendeleo na usalama wa wananchi.


Wananchi na wafanyabiashara sasa wanafanya kazi zao usiku bila kutumia vibatari. Tunaomba wananchi waendelee kutunza miundombinu hii muhimu kwa manufaa ya wote,” alisema Msiseme.


Kwa upande wake, Mzee Hashimu Akida, Diwani mstaafu na mzee wa mji wa Bagamoyo, alisema wananchi wamefurahishwa na mradi huo ambao umeleta mwanga, usalama na ajira kwa vijana.

Taa hizi zimependezesha mji wetu na kuongeza uhai wa shughuli za usiku. Watalii sasa wanatembea hadi saa nne usiku bila hofu,” alisema Mzee Akida.


Ameongeza kuwa enzi za ukoloni taa za barabarani zilikuwa pia zikitumika kuelekeza njia muhimu kama hospitali na sehemu zingene muhimu, hivyo akaiomba TARURA kuendeleza utamaduni huo ili kuongeza mvuto wa utalii katika mji wa kihistoria wa Bagamoyo.

No comments:

Post a Comment

Pages