NA DENIS MLOWE, MBARALI, MBEYA
BODI ya Maji Bonde la Rufiji kupitia Mradi wa NBS–USANGU imeanza rasmi zoezi la urejeshaji wa mito iliyokuwa imepoteza uelekeo wake wa asili au kukauka kabisa kutokana na kujaa mchanga, hali iliyosababisha changamoto kubwa kwa wananchi na kuathiri uzalishaji wa kilimo katika Bonde la Usangu.
Akizungumza baada ya ziara ya Kamati ya Uongozi wa Mradi iliyotembelea eneo la urejeshaji wa Mto Mlowo, Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Mhandisi David Munkyala, alisema mradi huo ni hatua muhimu katika kulinda rasilimali za maji na kurejesha ikolojia ya mito kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
“Kwa muda mrefu mito mingi Usangu imeharibika kutokana na shughuli za kibinadamu na mmomonyoko wa ardhi. Kupitia mradi huu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Serikali ya Japan, tunarejesha mifumo ya asili ya mito ili maji yaende kwenye mkondo sahihi,” alisema Munkyala.
Aliongeza kuwa urejeshaji wa Mto Mlowo utaimarisha upatikanaji wa maji kwa kilimo na mifugo pamoja na kupunguza migogoro ya matumizi ya rasilimali za maji.
“Lengo ni kuona wakulima wanapata maji ya uhakika, mifugo haili na kunywa maji kiholela kwenye vyanzo, na mazingira yanahifadhiwa ipasavyo,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa NBS–USANGU, David Muginya, alisema urejeshaji wa mito ni suluhisho la asili (Nature-Based Solutions) linalosaidia kuondoa athari za ukame na mafuriko, na kuongeza uzalishaji wa kilimo katika vijiji vinavyozunguka Bonde la Usangu.
“Wananchi wameshaanza kuona matokeo. Mito inarejea kwenye mikondo yake, na uzalishaji wa chakula utaboreshwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Muginya.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa mradi huo, akiwemo Said Juma na Simon Kitereja, walionesha kuridhika na hatua iliyofikiwa na kuhimiza wananchi kuendelea kulinda maeneo yaliyorejeshwa ili mradi huo uwe endelevu.
Wananchi nao walitoa maoni kuhusu manufaa ya hatua hiyo. Hamis Mwatenga, mkazi wa Kijiji cha Mwatenga, alisema urejeshaji wa Mto Mlowo umeanza kufufua matumaini ya wakulima waliokuwa wakikosa maji. Omary Makolo wa Kijiji cha Ilaji aliongeza kuwa mradi huo umeondoa hofu ya kupoteza mazao kutokana na mabadiliko ya mkondo wa mto.
Mradi wa NBS–USANGU ni sehemu ya juhudi za Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kutekeleza miradi ya uhifadhi na kuboresha mazingira kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali ya Japan, ikiwa na lengo la kulinda rasilimali za maji na kuinua maisha ya wananchi wa Bonde la Usangu.









No comments:
Post a Comment