Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Bagamoyo, Mhandisi Bernard Mwita akizungumza na waandishi wa habari Bagamoyo mkoani Pwani, kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Makurunge linalounganisha vijiji vya Makurunge na Malanzi, mradi uliogharimu zaidi ya Sh milioni 498. ziara hiyo ilifanyika Bagamoyo mkoani Pwani. PICHA: MIRAJI MSALA.
Mhandisi Msimamizi wa Miradi ya TARURA Bagamoyo, Philimo David, akizungumza na waandishi wa habari Bagamoyo mkoani Pwani jana kuhusu ujenzi wa daraja linalounganisha Makofia–Kimalang’ombe kwenye ziara ya kutembelea miradi hiyo. PICHA: MIRAJI MSALA
Na Miraji Msala, Bagamoyo
Wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo kupitia TARURA, zilizowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja.
Kaimu Meneja wa TARURA Bagamoyo, Mhandisi Bernard Mwita, amesema miradi hiyo imeboresha kwa kiasi kikubwa huduma za usafiri na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa vijijini.
Miradi hii imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wetu. Sasa wanapata huduma za kijamii kwa urahisi kipindi chote cha mwaka, tofauti na awali ambapo maeneo mengi yalikuwa hayapitiki hasa wakati wa mvua,” alisema Mhandisi Mwita.
Miongoni mwa miradi iliyokamilika ni daraja la miguu mitatu lenye urefu wa mita 16.4 katika barabara ya Milo, lililofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya shilingi 499.8 milioni, na limekamilika kwa asilimia 100.
Tunawaomba wananchi waendelee kutunza miundombinu hii, kwa kuwa ni mali yao na ni muhimu kwa maendeleo ya jamii,” aliongeza Mhandisi Mwita.
Mradi mwingine ni barabara ya Ruvu–Milo yenye kilometa 11, yenye madaraja makubwa mawili na makalvati minne, iliyogharimu shilingi milioni 253.6. Kukamilika kwa barabara hiyo kumeondoa changamoto ya usafiri, na sasa inapitika mwaka mzima.
Aidha, Mhandisi Philimo David, msimamizi wa miradi ya TARURA Bagamoyo, alisema wametekeleza pia mradi wa ujenzi wa barabara ya Makofia–Kimalang’ombe yenye kilometa 2 kiwango cha changarawe na daraja moja, uliofanywa na Lutavi Construction Company Ltd kwa gharama ya shilingi milioni 121.9, na umekamilika kwa asilimia 100.
Mradi huu umesaidia sana kupunguza changamoto za usafirishaji wa mazao na kuwafungulia wananchi fursa za kiuchumi. Wakulima sasa wanauza mazao yao kwa urahisi na kufika masokoni bila vikwazo,” alisema Mhandisi Philimo.
Mkazi wa Mkunguni, Bi. Cristina Kasimangi, alisema kukamilika kwa daraja hilo kumeondoa changamoto kubwa za usafiri hasa wakati wa mvua.
Sasa watoto wanaenda shule bila shida na wagonjwa wanafika hospitali kwa urahisi. Zamani tulikuwa tunavuka kwa mitumbwi, ilikuwa hatari sana,” alisema Bi. Kasimangi.
TARURA Bagamoyo imeahidi kuendelea kusimamia kwa karibu miradi yote ili kuhakikisha wananchi wanapata thamani ya fedha za kodi wanazochangia na kuimarisha zaidi miundombinu ya barabara wilayani humo.






No comments:
Post a Comment