Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENKI ya CRDB imeboresha huduma zake za Internet Banking kwa kuongeza ufanisi, kasi na urahisi wa kufanya miamala, hatua inayolenga kupunguza changamoto ambazo wateja wamekuwa wakikabiliana nazo wakati wa kutumia huduma hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Oktoba 4, 2026, Mkurugenzi wa Biashara na Matawi wa benki hiyo, Bonaventure Paul, amesema maboresho hayo yamezingatia mahitaji ya wateja wanaotaka kufanya miamala kwa haraka, urahisi na usalama.
Amesema benki hiyo imekuwa ikifuatilia changamoto zinazowakabili wateja wake na kuzifanyia kazi kwa lengo la kuhakikisha inatoa huduma zinazokidhi matarajio ya soko.
“Tunajua changamoto zilizokuwepo awali, lakini kama benki inayoongoza katika ubunifu, siku zote tunaangalia changamoto hizo na kuzifanyia kazi ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora zaidi.
“Mteja anachohitaji ni kufanya miamala yake kwa urahisi, haraka na kwa usalama. Mambo hayo yote yamezingatiwa katika maboresho haya,” amesema Paul.
Ameongeza kuwa mfumo mpya wa Internet Banking umeboreshwa katika ubora, uwezo na urahisi wa matumizi ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya wateja wanaotumia huduma hiyo.
Aidha, amesema huduma hiyo inawawezesha wateja kufanya miamala saa 24 kwa siku bila kuwekewa ukomo wa muda, tofauti na huduma zinazotolewa kupitia matawi ya benki ambayo hufanya kazi kwa saa maalumu.
Amesema maboresho hayo ni sehemu ya jitihada za CRDB kuendelea kutumia teknolojia kuboresha huduma za kibenki na kuwapa wateja urahisi zaidi katika kufanya miamala yao.







No comments:
Post a Comment