HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

November 17, 2026

KABOGO AWANOA WAHITIMU CHUO CHA PENTECOSTAL MBEYA, ASISITIZA MAARIFA NA UPAKO KATIKA HUDUMA

 

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Umisheni kutoka mkoani Dodoma Mchungaji Daima Amosi Kabogo ambaye amehubiri neno katika mahafali hayo ya 24 jijini Mbeya.

 

Na Lydia Lugakila, MBEYA

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Umisheni kutoka mkoani Dodoma, Mchungaji Daima Amosi Kabogo, amewataka watumishi wa Mungu kuendelea kujijengea maarifa na kuimarisha maisha yao ya kiroho kwa kuwa na upako, akisisitiza kuwa mambo hayo ni nguzo muhimu katika kufanikisha huduma ya Mungu.

Ametoa wito huo wakati akihubiri katika mahafali ya 24 ya Chuo cha Biblia cha Pentecostal Holiness Mission (PHM) Bible College Mbeya jijini Mbeya.

Mchungaji Kabogo amesema kuongeza maarifa si suala la sheria ya kanisa pekee, bali ni hitaji muhimu katika huduma ya Mungu, akieleza kuwa mtumishi anapaswa kuwa na uelewa wa kutosha wa kile anachokifundisha ili aweze kuwasaidia wengine kukua kiroho.

Mtumishi huyo wa Mungu amesema katika nyakati hizi zenye changamoto mbalimbali katika huduma za kiroho, kinachomtofautisha mtumishi mmoja na mwingine ni kiwango cha maarifa alichonacho pamoja na nguvu za Mungu zinazomwezesha kutekeleza wajibu wake.

Ameeleza kuwa mtumishi hawezi kufundisha jambo asilolijua, hivyo ni muhimu kujifunza, kuongeza uelewa na kuimarisha uwezo wa kuhudumu ili ujumbe anaoutoa uwe na msingi imara. 

Amesisitiza kuwa watumishi hawapaswi kukomea katika kiwango cha elimu walichofikia, bali waendelee kujifunza kwa kuwa kanisa linalojengwa katika msingi wa mafundisho sahihi huwa imara.

Mchungaji Kabogo Ameongeza  kuwa elimu pekee haitoshi bila maisha ya kiroho yaliyoimarishwa, akibainisha kuwa maarifa na upako vinapaswa kwenda pamoja katika kumwezesha mtumishi kutekeleza wajibu wake.

Katika hatua nyingine, amewapongeza wahitimu kwa kufikia hatua hiyo ya masomo na kuwataka kutumia elimu waliyoipata kuimarisha huduma zao na kuwa na mchango chanya katika kanisa na jamii.

Kwa upande wa taarifa ya maendeleo ya chuo iliyosomwa na mkuu wa chuo hicho Mchungaji Timoth Ibrahim Swai, imeelezwa kuwa chuo hicho kimefanikiwa kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kwa mwaka 2026, ikiwemo kusakafia vyumba vitatu vya ofisi na korido moja, kuweka dari, kufunga mlango mmoja, fremu tatu za ofisi, kununua na kufunga fremu nne za milango pamoja na madirisha matatu ya chuma.

Mchungaji Swai amesema kuwa pia  chuo kimefanikiwa kukusanya chakula kupitia majimbo na idara ya UWWM, yakiwemo majimbo ya Igale, Mbeya Mashariki na Mbeya 

Akisoma taarifa hiyo, Mkuu wa chuo hicho ameongeza kuwa chuo  kina malengo makubwa ya kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia ili kuwa sehemu bora ya kuwaandaa watumishi wengi wa Mungu watakaopata maarifa yenye tija katika huduma zao na jamii kwa ujumla.

Katika risala yao, wahitimu wameeleza kuwa chuo kilianzishwa mwaka 1996 katika Kanisa la Pentecostal Holiness Mission jijini Mbeya kikiwa na wanachuo 18, lakini kwa sasa kina jumla ya wanachuo 58 wanaosoma kwa mfumo wa kutwa na bweni.

Wamesema chuo hicho kimefanikiwa kuzalisha watumishi wengi wanaohudumu katika maeneo mbalimbali nchini, huku kikifanikiwa pia kuanzisha vyuo vingine viwili ambavyo ni Ukombozi kilichopo Dar es Salaam na Betheli kilichopo Mafinga mkoani Iringa.

Katika mahafali hayo, chuo kimehitimisha mafunzo ya stashahada na astashahada kwa wahitimu 45 kati ya wanachuo 58.

Wahitimu wameeleza kuwa lengo la chuo ni kuwafikia watumishi wa Mungu kutoka madhehebu mbalimbali kwa kuwapatia elimu ya Neno la Mungu ili kuwaimarisha katika huduma zao, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na uongozi kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Kwa upande wake, Mchungaji Josephat John Kibona ambaye alikuwa mgeni rasmi, ameishukuru bodi ya chuo kwa kumwalika katika mahafali hayo na kuwapongeza wahitimu kwa kukamilisha masomo yao.

Amesema si jambo dogo kwa mtu mwenye familia na majukumu mbalimbali kutenga muda kwa ajili ya masomo, hivyo amewapongeza wachungaji na watumishi walioamua kuongeza maarifa kupitia mafunzo hayo.

Pia ameipongeza chuo kwa maendeleo iliyofikia, akibainisha kuwa ongezeko la wanachuo kutoka 18 hadi 58 ni hatua inayodhihirisha ukuaji wa taasisi hiyo.

Amewataka wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa chuo kwa kuwahamasisha watumishi wengine kujiunga na masomo ili kuongeza maarifa na kuimarisha huduma zao.

Katika kuchangia maendeleo ya chuo, Mchungaji Kibona alichangia Sh. 450,000 kwa ajili ya upatikanaji wa viti 15 pamoja na Sh. 50,000 kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa kitanda huku wadau mbali mbali wakiungana naye katika kupunguza changamoto ya vitanda.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Idara Mchungaji John Aron Mwaigwisya amesema kwa mujibu wa katiba ya kanisa hilo, kanisa lina wajibu wa kuwapatia watu elimu ya neno la Mungu kabla ya kuwatuma kwenda kuhudumu katika maeneo mbalimbali ili waweze kuwa na mchango kwa waumini na jamii.

Mchg John  Mwaigwisya,amewataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kuwa mifano bora katika maeneo yao ya huduma na kuwa vielelezo kwa watu wanaowazunguka.

Aidha, amemshukuru mgeni rasmi kwa mchango wake katika kutatua baadhi ya changamoto za chuo.

Hata hivyo ameongeza kuwa upatikanaji wa vitanda pia umeanza kupata ufumbuzi kupitia michango ya mgeni rasmi, Mkurugenzi pamoja na watumishi wa Mungu na waumini wengine waliojitokeza kuchangia. 







 

No comments:

Post a Comment

Pages