HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

October 31, 2026

SIMBANKING YA CRDB YAONGEZA MIAMALA KWA ASILIMIA 33

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya CRDB imesema matumizi ya huduma zake za kidijitali kupitia SimBanking yameendelea kuongezeka, huku idadi ya miamala ikipanda kutoka milioni 8.8 hadi milioni 15, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 33.


 

Mafanikio hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kidijitali wa benki hiyo, Catherine Rutenge, wakati wa hafla ya kuwakabidhi washindi watano wa kampeni ya SimBanking Kimpango Wako zawadi ya safari ya siku tatu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Rutenge alisema kampeni hiyo imekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wateja, ambapo takribani watu milioni mbili wameshiriki kwa kufanya miamala kupitia huduma hiyo.

Alisema ongezeko la matumizi ya SimBanking linaonesha namna wateja wanavyozidi kuamini na kutumia huduma za kibenki kwa njia ya simu katika shughuli zao za kila siku.

Alifafanua kuwa kampeni hiyo imewezesha zaidi ya wateja 3,500 kujishindia zawadi mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 453 ambazo tayari zimetolewa.

Kwa mujibu wa Rutenge, washindi watano wa safari ya Serengeti kutoka mikoa mbalimbali nchini wamepatikana kupitia mfumo wa droo na watagharamiwa safari hiyo kwa asilimia 100 na benki hiyo.

Alisema safari hiyo itakayodumu kwa siku tatu itawapa washindi fursa ya kutazama wanyamapori, kufurahia mandhari ya hifadhi hiyo kupitia safari ya puto la angani pamoja na kupata malazi katika hoteli.

 

Aliongeza kuwa zawadi hizo zina thamani ya jumla ya Sh milioni 50 na ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha kidijitali pamoja na kutangaza vivutio vya utalii nchini.

Aidha, alisema kampeni hiyo inaendelea kutoa zawadi nyingine zikiwemo televisheni za kisasa kwa washindi 10 na jokofu la milango miwili kwa mshindi mmoja, kupitia miamala ya SimBanking inayofanywa kwa kutumia mawakala wa CRDB.

Alisema kwa sasa wateja wanaweza kupata asilimia 95 ya huduma za kibenki bila kufika katika matawi ya benki hiyo kutokana na maboresho ya huduma za kidijitali.

Katika hatua nyingine, Rutenge alisema kampeni hiyo inatarajia kuwazawadia washindi wengine watano safari ya kwenda barani Ulaya.



 

No comments:

Post a Comment

Pages