HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 16, 2024

Makamu wa Rais atoa maagizo Wizara ya Ardhi, Mamlaka za Serikali za Mitaa kuchukua hatua kulinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya bustani za kijani

 Na Jasmine shamwepu, Dodoma

MAKAMU wa Rais Dk. Philp Mpango, ameiagiza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mamlaka za Serikali za  Mitaa kuchukua hatua za makusudi kulinda maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya bustani za kijani ili yasiharibiwe au kubadilishwa matumizi.



Dk. Mpango amesema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akifungua Kongamano la Jukwaa Maendeleo Endelevu, kuhamasisha uwekezaji katika bustani za kijani kwa maendeleo endelevu.

Amesema, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Mamlaka za serikali za mitaa, zinapaswa kuchukua hatu za makusudi kulinda maeneo yote yaliyotengwa nchini kwa ajili ya bustani za kijani.

Amesema, kutokana na changamoto zilizopo maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya bustani za kijani katika miji na majiji nchini yameharibiwa na mengine kubadilishwa matumizi kinyume na mipango miji.

"Nitoe maelekezo yangu kwa wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi pamoja na mamlaka zote za serikali za mitaa kuhakikisha wanachukua hatua zikazo saidia kulinda maeneo haya ili yawe kama yalivyopangwa na yasibadilishiwe matumizi"alisema.

Dk. Mpango pia aliagiza maeneo yote ambayo yalitengwa na mamlaka kwa ajili ya bustani za kijani kupimwa na kuwekwa mipaka ili watu wasivamie na kubadili matumizi na kuondoa malengo mazuri ya kutuunza mazingira.

"Pia mamlaka za serikali za mitaa zihakikishe kuwa zinatunga sheria ndogondogo ambazo zitatumika kulinda maeneo haya ili yasiharibiwe wala kubadilishwa matumizi yake"alisema

Aidha, ameitaka  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kuanzisha tuzo maalum ya kushindanisha bustani bora za miji na majiji.

"Bustani hizi za kijani katika maeneo yote zinafaida kubwa sana kwani zinasaidia kutunza mazingira zinasaidia kuleta hewa safi hivyo tuzo hii itasaidia kuongezeka kwa bustani za kijani nchini na kuondoa hewa ya carbon"alisema

Vile vile, ametoa wito kwa sekta binafsi, Asasi za kiraia, mashirika na watu binafsi kuchangamkia fursa ya uanzishwaji wa bustani za kijani katika maeneo yao ili kushiriki kulinda mazingira lakini pia kujipatia kipato kama ilivyo katika mataifa mengine ya nje.

Kadhalika, aliuagiza mkoa wa Dodoma kuhakikisha kuwa kabla ya mwisho wa mwaka huu kuwa na bustani tatu za kijani.

"Naagiza kabla ya mwisho wa mwaka huu lazima hapa Dodoma kuwa na bustani za kijani tatu tusiishie kusifia bustani za nchi za nje tuu umefika wakati sasa na sisi kuwa na za kwetu ambazo zitakuwa kivutio kwa watalii na kuongeza kipato chetu"alisema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 56 ya watanzania wanaishi mjini hivyo kama hatua za makusudi hazitachukuliwa hali itazidi kuwa ngumu.

" Hivi sasa idadi ya watu wanaoishi mjini inaongezeka na hali ya joto inaongezeka kutoka na uharifu wa mazingira hivyo uwepo wa bustani hizi za kijani katika miji yetu kutasaidia kukabili hali hii"alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages