HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 20, 2013

24 WAITWA TAIFA STARS KUIVAA GAMBIA

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameita kambini wachezaji 24 kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu nchini humo.

Wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini Agosti 29 mwaka huu kabla ya saa 1 kamili usiku. Kambi ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa kwenye hoteli ya Accommondia jijini Dar es Salaam.

Makipa walioitwa katika timu hiyo Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Erasto Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na David Luhende (Yanga).

Viungo Khamis Mcha (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Dilunga (Ruvu Shooting), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Amir Kiemba (Simba), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga), John Boko (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na Juma Liuzio (Mtibwa Sugar).

RAMBIRAMBI MSIBA WA BARAKA KITENGE
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Yanga na Taifa Stars, Baraka Kitenge (74) kilichotokea leo mchana (Agosti 20 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Kitenge akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

Kitenge amefia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo alikuwa amelazwa akisumbuliwa na kansa ya uti wa mgongo. Enzi zake katika Yanga na Taifa Stas alicheza na wachezaji kama akina Athuman Kilambo na Abdulrahman Juma.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kitenge, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Yanga na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mipango ya mazishi inafanywa nyumbani kwa Marehemu, Yombo Vituka (Jet) jijini Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Kitenge mahali pema peponi. Amina

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages