Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Abbas Kandoro kuomboleza vifo vya watu 10
vilivyotokea Mbalizi, Mkoani Mbeya tarehe 29 Agosti, 2014 baada ya basi dogo la
abiria aina ya Toyota Hiace maarufu kama Daladala Na. T 237 BFB kugongana na
lori aina ya Tata Na. T 158 CSV. Katika
ajali hiyo, watu saba wengine walijeruhiwa na kukimbizwa hospitali kwa
matibabu.
“Nimesikitishwa
na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 10 na wengine saba kujeruhiwa
katika ajali hii iliyotokea siku chache baada ya ajali nyingine kutokea Mkoani
Tabora iliyoua watu 19 na wengine 81 kujeruhiwa”, amesema Rais
katika salamu zake.
Rais Kikwete
amesema mfululizo wa ajali hizi unaonyesha dhahiri kuendelea kuwepo kwa tatizo la
ukosefu wa umakini miongoni mwa madereva, hivyo jitihada zaidi zinatakiwa
kufanywa kusimamia kikamilifu Sheria ya Usalama Barabarani na kufuatiliwa kwa
karibu kwa mienendo ya wanaoendesha vyombo vya moto, ili ajali hizi ziweze kupunguzwa
na hata kudhibitiwa kabisa katika barabara zetu.
“Naomba upokee
salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana na ajali
hiyo, na kupitia kwako naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa wafiwa wote
kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao”Ameongeza.
Rais Kikwete amesema
anatambua machungu waliyo nayo wanafamilia, ndugu na jamaa wa watu waliopoteza
maisha yao kwenye ajali hiyo, lakini anawaomba wote wawe wavumilivu na wenye subira
wakati huu wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao.
“Ninawaombea
kwa Mola majeruhi wote wa ajali hiyo waweze kupona haraka na kurejea katika
hali zao za kawaida ili waweze kuungana
tena na familia, ndugu na jamaa zao”,
amemalizia
kusema Rais Kikwete katika salamu zake.
Imetolewa
na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
31
Agosti,2014
No comments:
Post a Comment