HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2017

WAZIRI MKUU AZINDUA SAFARI ZA ATCL DAR/DODOMA

 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia viongozi na wananchi wa Dodoma  baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma akitoka  uwanja wa ndege  wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam Januari 16, 2017 ikiwa ni uzinduzi wa Safari za ndege za Shirika hilo  kati ya viwanja viwili hivi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wafanyakazi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kabla ya kupanda ndege ya Shirika hilo kwenye uwanja wa Ngege wa Julius Kambarage Nyerere kwenda Dodoma  ikiwa ni uzinduzi wa safari za ndege za ATCL kati ya viwanja viwili hivyo,  Januari  16, 2017. 

DODOMA, TANZANIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Makao Makuu ya Nchi, Dodoma.

Akizindua safari hizo leo (Jumatatu, Januari 16, 2017) amesema safari hizo zitawezesha wafanyabiashara na wananchi wengine kutoka Dodoma na kwenda katika maeneo mengine kwa urahisi.

Amesema kuanzishwa kwa safari hizo ni moja ya utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais, Dkt.  John Magufuli za kufufua ATCL na kuboresha usafiri wa anga nchini.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa watumishi wa umma, wafanyabiashara na wananchi wa Dodoma kutumia ndege hizo kwa safari za kwenda katika maeneo mbalimbali kwani ni za uhakika na gharama zake ni nafuu.

“Tuna ndege nzuri. Tuzitumie kwenda katika maeneo mengine kwani gharama zake ni nafuu. Kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ni sh. 165,000, kwenda na kurudi ni  sh. 299,000,” amesema.

Amesema ndege nyingine kama hiyo inatarajia kuwasili nchini Juni mwaka huu jambo ambalo litaongeza idadi ya safari za ndege hizo nchini na maeneo mengine ya nchi jirani.

Naye Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma kutumia vizuri fursa hiyo ya safari za ndege za ATCL kwa kuwa utawawezesha kusafiri kwa muda mfupi tofauti na vyombo vingine vya usafiri.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Jordan Rugimbana ameshukuru kwa uanzishwaji wa safari hizo kwa kuwa zitarahisisha kutoka katika Makao Makuu ya nchi na kwenda katika mikoa mingine nchini.

Naye Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Malecela ameupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa namna anavyofanya kazi. Amefurahishwa na uanzishwaji wa safari hizo.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa ATCL. Kapten Richard Shaidi ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa ujio wa ndege hizo na kwamba hiyo ni moja ya mikakati ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ya kufufua ATCL.

“Hivi karibuni tunaanza kwenda nchi jirani. Mwakani tutapata ndege nyingine kubwa itakjayokuwa inafanya safari za masafa ya kati na ya mbali.
Naipongeza Serikali kwa kutoa ahadi na kuitekeleza kwani kutoa ahadi ni jambo rahisi ila utekelezaji wake ndiyo kazi. Lakini Serikali imeweza,” amesema.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Bw. Emmanuel Korosso amesema hivi karibuni shirika hilo linatarajia kuanza safari za kwenda katika miji ya Tabora, Songea, Mtwara, Mpanda, Mafia na Jiji la Tanga.

Akizungumzia kuhusu safari za Dodoma amesema zitafanyika mara mbili kwa wiki, siku ya Ijumaa na Jumatatu. Hata hivyo wanatarajia kuongeza safari hapo baadae.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, JANUARY 16, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages