Dande Contact

TEMBELEA BLOG HII KWA MATUKIO YA KILA SIKU-MOBILE +255 713 623 958 / +255 784 623 958 EMAIL dande15us@gmail.com

Halotel


CRDB

CRDB
.

Pages

MAGORI, WENZAKE, WATIMULIWA RASMI NSSF

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji NSSF, Crescentius Magori.

*Jumla 12, wakiwamo wanandoa


Na Mwandishi Wetu

BODI ya Wadhamini wa Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) imewafukuza kazi vigogo wake 12 waliosimamishwa kazi Julai mwaka jana, wakiwamo wanandoa.


Uamuzi wa bodi hiyo ulitolewa baada ya kikao chake cha kawaida cha 72 kilichoketi Juni 30, mwaka huu na kujiridhisha kwamba walihusika na makosa ya uzembe uliopindukia au kwa makusudi walishiriki kufanya ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi.

Waliofukuzwa kazi ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi, Yacob Kidula na mkewe, Amina Abdallah, aliyekuwa Meneja Utawala.

Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha, Ludovick Mrosso, aliyekuwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Chiku Matessa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Udhibiti, Hadhara na Majanga, Sadi Shemliwa.

Wakurugenzi wengine ni Pauline Mtunda, aliyekuwa Idara ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani na Crescentius Magori, aliyekuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji.

Watumishi wengine waliosimamishwa kazi ni mameneja ambao ni Abdallah Mseli aliyekuwa kwenye Idara ya Uwekezaji na Mhandisi John Msemo aliyekuwa Meneja Miradi.

Wengine ni Wakili Chedrick Komba aliyekuwa Meneja Kiongozi Mkoa wa Temeke, Mhandisi John Ndazi aliyekuwa Meneja Miradi na Ramadhan Nasib aliyekuwa Meneja Mkuu wa Usalama. Kutokana na hatua hiyo, bodi hiyo imetangaza nafasi za kazi ili kujaza nafasi hizo.

Hata hivyo, Mhasibu Mkuu wa shirika hilo, Davis Kalanje, aliyesimamishwa kazi pamoja na vigogo hao, jina lake halikuonekana kwenye orodha ya waliofukuzwa kazi.

Vigogo hao walisimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.

“Uchunguzi wa bodi hiyo umebaini kuwa watumishi hao kwa namna moja au nyingine ama kwa uzembe uliopindukia au makusudi walishiriki kufanya ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira. 

“Watumishi hao wameliingiza shirika katika hasara, madeni na upotevu wa fedha. Uchunguzi umebaini kuwa Sh. Bilioni 12 zilitumika katika miradi ambayo bado haijaanza.

“Matumizi ya Sh. Bilioni 43 kwa ajili ya mradi ambao ulikwishaanza na baadaye kusitishwa, shirika kuingia mikataba mibovu inayowanufaisha zaidi wabia na kuwa na gharama kubwa zisizoendana na uwezo wa mtiririko wa fedha wa shirika na kusababisha tatizo la ukwasi.

“Shirika kushindwa kukusanya zaidi ya Sh. Bilioni 20 kutokana na utoaji wa mikopo isiyofuata taratibu, shirika kufanya manunuzi ya viwanja bila kufuata utaratibu na kuna ambavyo vimevamiwa… viwanja vyenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 18 vina matatizo,” ilieleza sehemu ya tangazo hilo lililotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu.

Madai mengine yanayowakabili vigogo hao ni kulisababishia shirika kutekeleza miradi bila kufanya upembuzi yakinifu na shirika kutekeleza miradi ambayo gharama zake huongezeka zaidi ya mara tatu wakati wa utekelezaji.

Vigogo hao wanadaiwa kuongeza gharama za miradi bila kupata idhini ya mamlaka husika huku bodi hiyo ikiendelea kufuatilia urejeshwaji wa fedha hizo kwa kuzingatia taratibu stahiki na kusitisha miradi yote yenye mikataba mibovu.

“Bodi inapenda kuuhakikishia umma kwamba hali ya mfuko kwa sasa ni salama kwa maana ya kuweza kutimiza majukumu yake kwa wanachama na wafanyakazi wote wa mfuko. 

“Mwenendo wa ukwasi wa shirika umeimarika kutoka Sh. Bilioni 12 Aprili mwaka jana hadi Sh. Bilioni 354 Juni mwaka huu, hali inayoliwezesha shirika kulipa malimbikizo ya madeni mbalimbali. 

“Pia makusanyo ya michango ya wanachama yameongezeka kufikia wastani wa Sh. Bilioni 60 kwa mwezi kutoka Sh. Bilioni 42 kwa mwezi,” ilisomeka sehemu ya tangazo hilo.

Tangazo hilo lilieleza namna bodi ya wadhamini wa NSSF ilivyojizatiti kusimamia nidhamu kwa watumishi, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha, kufuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi na ajira.

Julai mwaka jana, bodi ya wadhamini ya shirika hilo liliagiza kusimamishwa kazi kwa vigogo hao ili kupisha uchunguzi, kubaini wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.

No comments:

Post a Comment