HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 08, 2018

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Kasongwa (kulia), akipokea madawati na vifaa vya ujenzi kutoka kwa Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat, katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mtonga. Benki hiyo ilitoa msaada wa madawati 100 na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh. Mil. 30. (Na Mpiga Picha Wetu).

NA MWANDISHI WETU
 
BENKI ya NMB, katikati ya wiki imekabidhi msaada wa madawati, vifaa vya afya na vifaa vya ujenzi yakiwemo mabati na mbao, kwa shule mbalimbali wilayani Korogwe na Kilindi mkoani Tanga, vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 60.
Pamoja na vifaa hivyo vya kupaulia, pia NMB imekabidhi madawati 200 kwaajili ya kupunguza uhaba wa madawati katika shule za wilaya hizo mbili.

Shule zilizofaidika na msaada huo kwa upande wa wilaya ya Korogwe ni Shule ya Msingi Mtonga (madawati 100), Shule ya Sekondari Semkiwa (viti 50 na meza 50) na Shule ya Msingi Kwasemangube mabati, kofia na misumari vyenye thamani ya Sh. Milioni 5.

Nyingine ni pamoja na Shule ya Msingi Kwamngumi (mabati yenye thamani ya Sh. Milioni 5), Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe (mabati ya Sh. Milioni 5) na Shule ya Msingi Kijungumoto ya Halmashauri ya Mji Korogwe (mabati ya Sh. Milioni 5).

Kwa upande wa wilaya ya Kilindi, Shule ya Sekondari Kimbe imepata viti na meza 100, Shule za msingi za Mafisa, Nkama na Songe, zimepata mabati yenye thamani ya Sh. Milioni 20. Pia, NMB imetoa vifaa tiba kwa zahanati mbili kila moja Sh. Milioni 5 na vifaa vyote kuwa na gharama ya Sh. Milioni 30.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Kasongwa, aliishukuru NMB kwa msaada huo wilayani kwake na kusema utawasaidia kukabiliana na changamoto za uhaba wa madawati na vifaa vya ujenzi wa madarasa kwenye sekta ya elimu.

Kasongwa alisema pamoja na maendeleo makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwenye Sekta ya Elimu kwa elimu bila malipo, bado ni muhimu wadau kuchangia elimu ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo kwa sasa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo, alisema vifaa tiba na madawati walivyopewa na Benki ya NMB, vitasaidia kuboresha miundombinu ya shule na kuboresha afya za wananchi.

Naye Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat, alisema NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi kwa kujikita zaidi kwenye elimu kwa kutoa madawati na viti, huku kwenye sekta ya afya wakichangia vitanda, magodoro na kusaidia majanga yanayoipata nchi yetu.

No comments:

Post a Comment

Pages