HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 12, 2018

Watanzania washindwa kutamba Beirut Marathon

MBIO za Blom Bank Beirut Marathon zimerindima jijini Beirut, Lebanon huku ikishuhudiwa wawakilishi wa Tanzania wakishindwa kutamba.

Mbio hizo zinazotambuliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), ‘Silver Label’ zilishirikisha wanariadha 1,479 kwa upande wa Km. 42 ‘Full Marathon kutoka mataifa mbalimbali Duniani.

Tanzania iliwakilishwa na wanariadha wawili, Samson Lyimo na Glory Makula, ambao walipata fursa hiyo chini ya ufadhili wa Kampuni ya vinywaji baridi ya SBC Tanzania Limited, baada ya kufanya vema katika mbio za Rotary Dar Marathon zilizofanyika Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa wanawake Full Marathon, Makula alishika nafasi ya 17 akitumia saa 2:56.49.

Katika Kilomita 5 za mwanzo alitumia dakika 18:6, Kilomita 15 alitumia dakika 59:03, Kilomita 20 saa 1:20.14, Kilomita 30 alipita akitumia saa 2:03.04 na Kilomita 35 saa 2:24.47 kisha kumaliza kwa muda huo wa saa 2:56.49.

Mshindi aliibuka Medine Armino wa Ethiopia aliyetumia saa 2:29.30 akifuatiwa na Nazret Gebrehiwet wa Eritrea 2:29.30 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Muethiopia, Selamawit Tsegaw saa 2:31.40.

Kwa upande wa wanaume mshindi aliibuka Mohamed El Aaraby kutoka Morocco aliyetumia saa 2:10.41 akifuatiwa na Mganda Felix  Chemonges 2:11.54 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Deresa Ulfata wa Ethiopia aliyetumia saa 2:12.31 huku Mtanzania Samson Lyimo matokeo yake yakifutwa.

Kwa matokeo hayo, wanariadha hao wa Tanzania wameshindwa kufikia muda wa kufuzu kwa mashindano ya Dunia huko Doha, Qatar mwakani.
Wawakilishi hao wa Tanzania wanatarajiwa kurejea nchini kesho.

No comments:

Post a Comment

Pages