HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 19, 2020

THRDC yatembelea mashirika mbalimbali yanayotetea haki za binadamu


Na Janeth Jovin

Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa akiwa na Ofisa Dawati wa Wanachama wa mtandao huo, Joyce Eliezer wametembea mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu nchini.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam ilieleza kuwa, Olenguruma  akiambatana na  Eliezer walitembelea mashirika hayo kwa nyakati tofauti.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa juzi Olengurumwa akiambatana na Eliezer  walitembelea Shirika la Wasaidizi wa Kisheria, Morogoro Paralegal Center (MPLC).

Ilieleza kuwa MPLC ni taasisi inayojihusisha na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria Bure kwa jamii, huku makundi makubwa yanayohudumiwa yakiwa ni wanawake, watoto na makundi maalum.

“Shirika hilo limejikita kufanya kazi katika mkoa mzima wa morogoro na  limefanikiwa kuanzisha na kuratibu  vituo  vya wasaidizi wa kisheria katika wilaya saba mkoani humo.Pamoja na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria taasisi hii imekuwa ikiendesha mradi wa kuwawezesha wanawake kusimamia na kumiliki Ardhi,” ilieleza taarifa hiyo.

Hata hivyo taarifa hiyo ilieleza, Olenguruma baada ya kutembelea taasisi hiyo na kusikiliza changamoto zinazowakabili, ameiasa taasisi ya hiyo kuendeleza mahusiano hayo mazuri na serikali ili kuendelea kuifikia jamii kwa upana na kuwawezesha wananchi kupata usaidizi wa kisheria pamoja na haki mbali mbali ambazo zimekuwa zikipotea.

Naye Eliezer ameishauri taasisi hiyo kutumia kituo cha televisheni cha Watetezi TV, kuibua baadhi ya changamoto zinazowakumba watetezi wa haki za binadamu ili kufanikisha utatuzi wa haraka pamoja na kuionyesha jamii kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na Watetezi hao kwa upana zaidi.

Aidha taarifa hiyo iilieleza Olengurumwa na Eliezer wametembelea pia Shirika la  Empower Society Transform Lives (ESTL) ambalo linajihusisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu,

“Shirika hili limejikita kufanya kazi katika mkoa mzima wa Singida na wilaya zake na  limefanikiwa kuisaidia jamii katika uwanda wa afya, elimu, mazingira na jinsia.

Pamoja na kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na ESTL bado kumekuwa na changamoto mbali mbali ambazo shirika hilo limekuwa likikutana nazo ambazo ni pamoja na Changamoto ya fedha ni kikwazo katika utekelezaji wa baadhi ya kazi za utetezi, tunashindwa kuwafikia wahitaji wote kwa wakati" alieleza Joshua Lisu, Mkurugenzi wa taasisi hiyo

Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa, baada ya kusikiliza kazi, changamoto, fursa na mafanikio yaliyofikiwa na taasisi ya ESTL, Olengurumwa ameishauri taasisi hiyo kujenga misingi ya taasisi ikiwa ni pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya pesa za wafadhili kwa maendeleo endelevu ya shirika.

Pia viongozi hao wa THRDC walifanikiwa kulitembelea shirika la Child watch Tanzania ambalo linajihusisha na utetezi  na ulinzi wa haki za mtoto mkoani Singida hasa likijikita katika kutokomeza usafirishaji haramu wa binadamu hasa watoto. 

“Mbali na kazi za utetezi wa haki za binadamu shirika hilo limekuwa likifanya kazi mbali mbali za ujasiriamali ili kuwawezesha vijana wadogo wanaoishi katika mazingira hatarishi kuondokana na hatari za kuingia katika biashara haramu ya usafirishaji watu ambao unazaa ukatili wa kijinsia.

Shirika la Child Watch Tanzania linaendesha mradi wa ufugaji nyuki kwa vikundi vinne vya vijana 40 ambapo  kuna mizinga 160 kupitia mradi huu ambao kwa sasa umefikia katika hatua ya uvunaji,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha ilieleza kuwa shirika hilo limekuwa inafanya kazi upande  wa afya ambapo inafanya kazi ya kujenga uwezo wa mashirika baadhi yaliyochaguliwa na wataalamu wa afya hasa katika upande wa kupambana na malaria chini ya mpango wa uwezeshaji mashirika kujua kwa undani kuhusu  Global Fund na hasa ugonjwa wa malaria.

1 comment:

  1. Hii ni hatua nzuri sana ya kuwatia moyo wanachama wa THRDC, kwani wanachama wanajifunza kitu tika staffs ya THRDC na staff wanajifunza toka kwa wanachama pamoja na mazingira ya kijamii.

    ReplyDelete

Pages