HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 19, 2012

MBUNGE WA ZAMANI AFARIKI DUNIA


Marehemu Siraju Kaboyonga enzi za uhai wake

DAR ES SALAAM, Tanzania

Mbunge zamani wa Tabora Mjini, Siraju Juma Kaboyonga (CCM), amefariki dunia jana jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia jijini Dar es Salaam leo, kaka wa marehema ambaye ni msemaji wa familia, Haji Kaboyonga, alisema kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo.

Haji alisema kuwa mdogo wake alikuwa mtu muhimu katika jamii na familia hasa katika masuala ya  ushauri ambapo  mauti yamemkuta huku msaada wake ukihitajika.

Alisema kuwa mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake Sinza Mori na mwili wa marehemu Kaboyonga unatarajiwa kuzikwa leo baada ya sala adhuhuri katika makaburi ya kisutu jijini Dar es Salaam.

Marehemu Kaboyonga hadi mauti yanamkuta alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
Kaboyonga enzi ya uhai wake alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo uwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa shirika la Hifadhi ya Taifa (NSSF), Meneja wa Kanda ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB).

Haji alisema kuwa marehemu ameacha watoto 12 na  wajane wawili.
Aidha Rais Jakaya Kikwete, amemtumia Salamu za rambirambi Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka, kwa kuondokewa na Mwenyekiti wake.

“Nimepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Siraju Juma Kaboyonga ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya SSRA na amefanya kazi kwa muda mfupi kabla mauti hayajamkuta”, alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema kuwa alimfahamu Marehemu alikuwa mtumishi mwenye uwezo mkubwa aliouonyesha dhahiri kipindi alichokuwa Mbunge aliweza kuwatumikia kikamilifu Wananchi wa Jimbo la Tabora Mjini na Umma wa Watanzania.

Rais Kikwete alisema kuwa uwezo aliokuwa nao ulimuwezesha kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa SSRA na mchango wake uliweza kuonekana dhahiri.

Aidha aliomba salamu hizo pia zifikishwe kwa familia ya Marehemu kwa kupotelewa na Kiongozi, na mhimili madhubuti wa familia.

No comments:

Post a Comment

Pages