Na Bryceson Mathias
Watafsiri wa Milio ya Wanyama na ndege wanasema, Mbwa anapobweka, eti huwa analia akiuliza “Kwa nini Tabu ni Mji huu, huu-huu- huu kila sikuu?
Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko ya Wakulima wa miwa kutoka vyama sita wa Bonde la Ruhembe, wilayani Kilosa, walioazimia kuacha kulima miwa kufuatia hatua ya Kampuni ya Sukari ya Ilovo, kupunguza bei ya miwa kutoka Sh 69,000 hadi Sh 62,889 kwa tani.
Vilio vya namna hiyo havikuanza jana bali vimekuwepo muda mrefu, hususani muda mchache baada ya wanaoitwa wawekezaji kupewa viwanda vya sukari kwa madai kwamba wataongoza tija, kuwapatia wafanyakazi na wakulima kipato kizuri na kulipatia Taifa Maendeleo.
Mbali na Wakulima kutoa msimamo katika mkutano uliofanyika Kata ya Kidodi ulioshirikisha viongozi wa vyama vya wakulima wa miwa, imebainika Wimbo wa Serikali wa Uwekezaji kuleta Tija, kipato kwa Wafanyakazi , Wakulima na Maendeleo kwa Taifa, Una kasoro .
Mwenyekiti wa Muungano wa vyama hivyo,Wenslaus Gwira, alisema anguko la bei kwa tani moja ya miwa, ni sawa na asilimia 10 ya bei ya miwa iliyokuwa awali, akidai, jitihada za kuonana na uongozi wa Ilovo, ili kutatua tatizo hilo, ziligonga mwamba.
Meneja wa ILOVO Don Carter, alidai kushuka kwa bei ya miwa kumetokana na kutokuwepo kwa soko la Sukari hapa nchini na kwamba hali hiyo, imechangiwa na Serikali kutoa fursa ya kuingiza sukari kutoka nje ya nchi.
Hivi ni kweli soko la sukari nchini halipo au tunababaishana na kuwafanya watanzania kichwa cha mwenda wazimu ili kujifunzia kunyoa? Wananchi wamekuwa wakihaha kuisaka Sukari hadi kufikia kununua kwa Sh. 3,000/- halafu mtu anafikia kusema nchini hakuna soko la sukari!!
Uongo wa wazi kama huu!! Haulitakii Mema Taifa letu, na kama alivyosema Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, watu wa namna ya Menjeja Wa Kiwanda Sukari ILOVO,wanatakiwa wapewe masaa 24 warudi kwao na kiwanda kirudishwe kwa wananchi.
Hivi Menjeja wa ILOVO, anaweza kusema uongo kushuka kwa bei ya miwa kumetokana na huhaba wa soko la Sukari nchini na viongozi wa Serikali na Waziri mwenye dhamana wakakaa kimya? Basi ni ukweli!
Kama ni kweli, ni nia ya Serikali iingize sukari kwa wingi, wakulima wakose bei nzuri wawe maskini? La hasha! Ninachojua kulikuwa na mafisadi walificha Sukari kwa ajili ya kujinufaisha, wananchi walipobaini mbadala wa Asali kwenye chai, imewaozea!
Serikali na Mawaziri wenye dhamana, sasa waelewe wananchi wana uelewa mkubwa kuliko serikali yao wamekomazwa na matizo, hivyo yanapowafika kooni wanatafuta njia mbadala kwa kutokana na kuchoshwa na Ufisadi na umangimeza wa viongozi.
Kama ilivyokuwa kwenye udanganyifu wa dawa feki za VVU kulikopoteza nguvu kazi ya watu, sasa wananchi hawahadaiki tena kumnufaisha Muasisi wa Babu wa Loliondo, bali wamegundua Unga wa Ubuyu na tiba ya Mti huo inayodaiwa kuoneza CD4, Mavidonge yatawaozea
Wananchi wengi sasa wamebaini kutumia Asali kuunga kwenye chai au Uji majumbani, ambapo walalahoi nao wanamudu, hali ambayo kwenye majani ya chai wengi wameyazira na kuunga Majani ya Mchaichai ambao una harufu nzuri.
Kutokana na manyanyaso na kuambukizwa umaskini, wananchi sasa katika viwanda karibu vyote vya Sukari, wakulima wamefikia uamuzi kuachana na kilimo cha Miwa kutokana na kudaiwa kinaendelea kuwapa umasikini wa kipato na kugeukia mazao mengine yenye tija.
Omary Abdallah ambaye ni kiongozi wa Chama cha Wakulima wa Miwa Kidodi alisema, wameamua kufanya hivyo ili kulinda maslahi ya wakulima wa miwa hapa nchini, na kuongeza, kuwa, suala hilo sasa limeingiliwa na siasa,, hivyo wanageukia mpunga, Mahindi.
Licha ya Meneja Mkuu wa ILOVO, Carter, kudai kushuka kwa bei ya miwa kumetokana na Serikali kuruhusu kuingizwa sukari ya nje, na kwamba sasa kuna zaidi ya tani 40,000 zimerundikana; Je ilikuwa wapi muda wa shidai?.
KWA MAWASILIANO
0715-933308
No comments:
Post a Comment