HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 08, 2013

TFF BADO YASISITIZA KUMUONA WAZIRI MUKANGARA


RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amemshukuru Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara kwa kukubali ombi la Shirikisho la kutaka kukutana naye kwa mazungumzo na kumsihi asitishe hatua anazodhamiria kuchukua hadi hapo kikao hicho kitakapofanyika.

Waziri Mukangara ameiagiza TFF kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya katiba ifikapo tarehe 15 Aprili 2013 na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ifikapo tarehe 25 Mei 2013 na kwamba tamko la TFF kutekeleza maagizo hayo liwe limetolewa katika muda wa siku tano zinazoishia Jumatatu (Machi 11, 2013).

Katika barua pepe ambayo amemuandikia Waziri ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, Rais Tenga ameeleza kuwa alikwenda ofisini kwake tarehe 7 Machi 2013 kujaribu kumuona lakini akaambiwa amesafiri, hivyo kuomba kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye pia hakuwepo ofisini na hatimaye akakutana na Naibu Katibu Mkuu.

Katika barua hiyo pepe, Rais Tenga ameeleza madhumuni ya kutaka kuonana na Waziri Mukangara kuwa ni kwanza “kukushukuru kwa kukubali kuonana na ujumbe wa TFF ulioongozwa na mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji, Bw. Alex Mgongolwa, akiongozana na Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Angetile Osiah, jana tarehe 6 Machi 2013.


“Kukushukuru kwa kukubali kukutana nasi tena siku ya tarehe 19 Machi, kwa ajili ya mazungumzo juu ya maagizo yako. 


“Kukuarifu kuwa nimepokea maagizo yako uliyoyatoa jana kupitia kwa Mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji na kwa njia ya barua; na
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”


Tenga, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) aliondoka jana (Machi 7 mwaka huu) kwenda Marrakech, Morocco kuhudhuria kikao cha kamati hiyo na pia Mkutano Mkuu wa CAF ambao umepangwa kufanyika Machi 10 mwaka huu ukihusisha pia ajenda ya uchaguzi wa rais.

KAIJAGE KOCHA MPYA TWIGA STARS

ROGASIAN Kaijage ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya wanawake, Twiga Stars baada ya kocha wa zamani, Charles Boniface Mkwasa kujiuzulu katikati ya mwaka jana.

Mkwasa, ambaye alikuwa nyota wa Yanga na Taifa Stars, alijiengua kufundisha timu hiyo aliyoiongoza kwa muda mrefu, baada ya Twiga Stars kuondolewa katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika nchini Equatorial Guinea.

Twiga ilipata bao muhimu la ugenini jijini Addis Ababa ilipofungwa na wenyeji wao Ethiopia mabao 2-1, lakini ikiwa na matumaini ya kutumia vyema bao la ugenini ilijikuta ikilala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa katika mchezo wa marudiano na hivyo kukosa tiketi ya kurudi tena kwenye fainali hizo.

Kaijage ambaye kwa sasa anajihusisha na mradi wa vijana (grassroots) pamoja na programu nyingine za kukuza vipaji zilizo chini ya TFF, aliteuliwa na Kamati ya Ufundi ya TFF kufanya kazi hiyo na ameita kikosi cha Twiga Stars kwa mazoezi ya siku kumi kuanzia Machi 10 hadi 23 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Wachezaji walioitwa ni Amina Ally (Lord Barden), Asha Rashid (Mburahati Queens), Aziza Mwadini (Zanzibar), Esther Chabruma (Sayari), Esther Mayalla (TSC Academy), Etoe Mlenzi (JKT), Evelyn Sekikubo (Mbarahati Queens), Fatuma Bushiri (Simba Queens), Fatuma Mustafa (Sayari) na Fatuma Omari (Sayari).

Flora Kayanda (Tanzanite), Hamisa Athuman (Marsh Academy), Hellen Maduka (Bujora), Hellen Peter (JKT), Irene Ndibalema (TSC Academy), Maimuna Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Tanzanite), Mwanaidi Tamba (Mburahati Queens), Mwanahamis Omari (Mburahati Queens) na Mwapewa Mtumwa (Sayari).

Nabila Ahmed (Marsh Academy), Nasiria Hashim (Zanzibar), Pulkeria Charaji (Sayari), Rukia Khamis (Sayari), Semeni Abeid (Tanzanite), Sharida Boniface (Makongo Sekondari), Sophia Mwasikili (Luleburgaz Gucu Spor, Uturuki), Theresa Yona (TSC Academy), Vumilia Maarifa (Evergreen) na Zena Khamis (Mburahati Queens).

YANGA, TOTO AFRICANS KUUMANA DAR
MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Machi 9 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo vinara Yanga watakuwa wenyeji wa Toto Africans kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwamuzi wa mechi hiyo namba 135 atakuwa Andrew Shamba kutoka Pwani akisaidiwa na Abdallah Mkomwa na Abdallah Rashid pia wote kutoka Pwani. Kamishna ni Salim Singano kutoka Tanga wakati Mtathmini wa waamuzi ni Alfred Lwiza.

Nayo Polisi Morogoro itakuwa mgeni wa Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Azam katika mechi hiyo namba 136 na nyingine mbili zinazofuata itakuwa bila kocha wake Steward John Hall ambaye Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia mechi tatu.

Charles Komba kutoka Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 136 itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani.

Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa (Machi 10 mwaka huu) ambapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utashuhudia mechi kati ya Simba na Coastal Union ya Tanga. Waamuzi wa mechi hiyo ni Martin Saanya akisaidiwa na Jesse Erasmo na Vicent Mlabu wote kutoka Morogoro.

RHINO, KANEMBWA ZASAKA TIKETI VPL
KINDUMBWENDUMBWE cha Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kinaendelea kesho (Machi 9 mwaka huu) katika makundi yote matatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu yakiwa kwenye mechi za Rhino Rangers ya Tabora na Kanembwa JKT ya Kigoma.

Timu hizo ndizo ziko katika nafasi nzuri ya kupata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao kutoka kundi hilo la C. Tayari Mbeya City ya Mbeya na Ashanti United ya Dar es Salaam zimeshapata tiketi za kucheza VPL msimu ujao kutoka kundi A na B.

Rhino Rangers itaikaribisha Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, wakati Kanembwa JKT itakuwa mgeni wa Pamba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mechi nyingine za kundi C ni Mwadui vs Polisi Tabora (Kambarage, Shinyanga), na Morani vs Polisi Mara (Kiteto, Manyara). Mechi za kundi A ni Majimaji vs JKT Mlale (Majimaji, Songea), Mkamba Rangers vs Mbeya City (Sokoine, Mbeya) na Polisi Iringa vs Burkina Faso (Samora, Iringa).

Mshikeshike ya kundi B ni Ndanda vs Ashanti United (Nangwanda Sijaona, Mtwara), Villa Squad vs Green Warriors (Karume, Dar es Salaam), Polisi Dar vs Transit Camp (Mabatini, Mlandizi) wakati Tessema na Moro United zitacheza Machi 10 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages