HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 17, 2013

Aliyesababisha kifo cha askari wa usalama barabarani katika Msafara wa JK Dar afikishwa mahakamani Iringa kwa utapeli


Mfanyabiashara  wa Mbeya ambae ndie  alikuwa  dereva wa gari namba  T.328 BML aina ya Land Lover Discovery na kusababisha kifo cha askari mwenye namba  WP 2492 Coplo Elikiza Nnko wakati wa  msafara  wa Rais Jakaya  Kikwete  jijini Dar es Salaam  hivi karibuni , amefikishwa leo katika mahakama ya Mwanzo Bomani Iringa  kwa tuhuma za kujipatia gari aina ya fuso yenye thamani ya Tsh milioni 30 kwa njia ya udanganyifu  kutoka kwa mwanamke  Venannsia Sanga  wa Iringa (Picha na Francis Godwin)



Na  Francis Godwin, Iringa


MFANYABIASHARA mkazi  wa Mbeya ambae alikuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T.328 BML aina ya Land Lover Discovery na kusababisha kifo cha askari mwenye namba  WP 2492 Coplo Elikiza Nnko wakati wa  msafara  wa Rais Jakaya  Kikwete  jijini Dar es Salaam ,amefikishwa mbele ya hakimu  wa mahakama ya Mwanzo Bomani mjini Iringa kwa tuhuma  za  kujipatia gari lenye thamani ya Tsh milioni 30 .

Mfanyabiashara  huyo Jackson Simbo Stivin(45) alifikishwa mahakamani jana akituhumiwa  kujipatia gari aina ya fuso lenye thamani ya Tsh milioni 30 ambalo ni mali ya mfanyabiashara  wa mkoani Iringa  Venansia Sanga.

Akisoma shtaka  hilo  hakimu  wa mahakamani  hiyo ya Mwanzo Bomani  Mheshimiwa  Alois Masua alisema  kuwa  mtuhumiwa  huyo anadaiwa  kutenda  kosa  hilo Septemba 4 mwaka  2012 katika  eneo la Miyomboni mjini Iringa .

Masua   alisema  kuwa  mtuhumiwa  huyo baada ya  kutenda  kosa  hilo alitoweka na kujificha katika mikoa mbali mbali hapa nchini .

Hata  hivyo  alisema  kuwa  mlalamikaji katika  shtaka  hilo  baada ya  jitihada za kumtafuta  kushindikana ndipo alipofika mahakamani  Februari 15 mwaka  huu  kufungua kesi namba 61 /2013 kuhusiana na mtuhumiwa  huyo.

Alisema  kuwa  kutokana na  kufunguiliwa kwa kesi hiyo jeshi la  polisi kwa kushirikiana na mlalamikaji  waliendelea kumsaka mtuhumiwa  huyo bila mafanikio na baada ya kutokea ajali iliyosababisha  kifo cha askari  huyo  wa  usalama barabarani jijini Dar es Salaam katika msafara  wa Rais Kikwete ndipo mtuhumiwa huyo alipokamatwa baada ya  picha yake  kuonekana katika vyombo vya habari .

Mtuhumiwa  huyo amekana kosa  hilo ambapo  mahakama hiyo imesema    kuwa dhamana yake  ipo  wazi na kuwa mdhamini anapaswa kusaini hati ya dhamana ya yenye  thamani ya Tsh. milioni 15 masharti ambayo yalitimizwa na wadhamini na mfanyabiashara  huyo kutolewa kwa dhamana hadi Aprili 25 kesi  hiyo itakapotajwa  tena.

Wakati  huo  huo ndugu  wa mfanyabiashara  huyo walionyesha  kuwazuia  wanahabari  kumpiga  picha  wala kuandika  habari  hiyo kwa madai  kuwa ni habari  ndogo ambayo jamii  haipaswi  kuijua na kumtaka mfanyabiashara  huyo  kujifungika  sura yake na kuondoka na msafara  wa magari mawili ya kifahari katika mahakamani hiyo .

No comments:

Post a Comment

Pages