HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 16, 2013

CCM NI WAUMINI WA FALSAFA YA 'MKUKI KWA NGURUWE'



Na Bryceson Mathias
MARA kadhaa tumesikia,Chama cha Mapinduzi (CCM), kimekuwa na tabia ya kuwakumbatiia viongozi wake wanaobainika na maovu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutosoma mapato na matumuzi kwa mujibu sheria za Serikali za Mitaa (TAMISEMI), lakini kwa wapinzani kinakubali kirahisi.
Kwa mujibu wa uchunguzi niliofanya katika vitongoji, vijiji na kata nchini, Wenyeviti wengi  Serikali za Mitaa na Watendaji wao, wameshindwa kuendana na Sheria ya TAMISEMI, kwa sababu wengi wana zaidi ya miaka miwili hawajasoma mapato na matumizi.
Sheria ya TAMISEMI inamtaka kiongozi asome mapato na matumizi kila baada ya miezi mitatu, na asiposoma kwa miezi mitatu mfululizo, serikali inakuwa imepoteza sifa, wananchi wanaweza kuitisha Mkutano wa Hadhara kuchagua uongizi mbadala.
Serikali nyingi za vijiji za namna hiyo nchini, zimepoteza sifa kutokana na viongozi wake kutosoma mapato na matumizi na nyingine viongozi wake kukumbwa na kashfa kubwa za matumizi mabaya ya fedha lakini bado zinakumbatiwa kwa Udi na Uvumba.
Imebainika, serikali ambazo wananchi wake wamezikataa kwa kutosomewa mapato na matumizi au kwa viongozi hao kukumbwa na matumizi mabaya, na hatimae CCM kuzikingia kifua hata kwa mabomu ya machozi ya polisi, basi serikali hizo zina maslahi binafsi na watawala.
Imefahamika, kijijini hapo kunaweza kukawa na uwekezaji wa kiongozi mkubwa (Kigogo) wa Serikali, CCM, vyombo vikuu vya dola,  hata watu ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara wakubwa wenye kauli serikalini au CCM.
Ukichunguza na kufuatilia kwa karibu, utabaini serikali hizo zinapong’olewa na wananchi kwa sababu ya kukosa uadilifu, wananchi hupata ushindani mkubwa na mikutano yake kutawaliwa hata na risasi za moto, mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na virungu hadi kulemaa, ambapo madai na haki yao halisi hutupwa.
Upembuzi uliofanywa katika vijiji vya wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro, umeonesha kuwa Mvomero chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Sarah Linuma, inaongoza kwa viongozi wake kukaimishwa, kutokana na wahusika kukumbwa na kashfa hizo.
Lakini, viongozi wenye dhamana ya kusimamia mustakabali huo; kwa makusudi wamekuwa vipofu - hawaoni, wamekuwa viziwi -  hawasikii malalamiko ya wananchi kukiukwa kwa sheria hizo, badala yake wamewabeba na kuzirudisha au kukaimisha serikali hizo.
Mifano Hai; Wanakijiji wa Sagamaganga wilayani Kilombero, hivi karibuni waliung’oa Uongozi wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Mohamed Mkupika (CUF), kwa tuhuma mbalimbali, hatua iliyoridhiwa na kusimamiwa na Mkuu wa Wilaya, Hassan Masala, kwa kupiga kura, lakini wananchi wa Ruaha wanayimwa haki yao kwa Tuhuma hizo hizo.
Maswa, Mkuu wa Wilaya, Abdalah Kihato, hivi karibuni alivunja mkutano  wa kitongoji cha Biafra, uliotaka kumng’oa Mwenyekiti, Hassan Tindo, kwa tuhuma mbalimbali, ambapo kila anapotaka kung'olewa, hukimbilia CCM na kwa DC Kihato.
Wilaya ya Mvomero, Mkurugenzi Linuma anayedaiwa kutafuna mamilioni, na hatimaye kukataliwa na Baraza la Madiwani; Licha ya tuhuma za manoti hayo, uongozi wake unaongoza kuwabeba na kuwakaimisha Wenyeviti wa namna hiyo nchini.
Mtendaji Kata wa Mhonda, Emily Mjenja (CCM), kwa maagizo ya Linuma, alimfungulia kesi Mwenyekiti wa Muda, Niko Mbelwa (CHADEMA), aliyechaguliwa na wananchi baada ya kukataa kumpa mihuri na vitendea kazi vya Ofisi ya Kijiji, kutokana na wananchi kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM; Tusemeje?

Hapa ndipo napoona kuwa viongozi wa ngazi mbalimbali wa CCM ni waumini wazuri wa falsafa ya Mkuki kwa nguruwe, kwa binaadamu mchungu. Kwa nini ikumbatie baadhi ya wakosaji huku ikiwatimua wengine kwa makosa kama hayo hayo?
Maoni, maswali ama ushauri kwa mwandishi, wasiliana naye kwa barua pepe: nyeregete@yahoo.co.uk
Simu namba: 0715 933 308

No comments:

Post a Comment

Pages