Na Elizabeth John
TASNIA ya muziki wa Hip hop nchini, imepata pengo kubwa
baada ya kumpoteza nyota wa muziki huo, Albert Mangwea ‘Ngwea’, aliyefariki
juzi akiwa Afrika Kusini alipoenda kwaajili ya kufanya shoo.
Ngwea aliondoka nchini mwezi uliopita alialikwa kafanya
shoo nchini humo ambayo aliifanya wiki tatu zilizopita, jana alitegemea kurejea
nchini.
Kwa mujibu wa Arusha255 Blog, baba mdogo
wa marehemu mzee Mangwea ambaye yuko Mbinga mjini Songea, amesema kuwa
wamekubaliana na kaka yake mkubwa yaani baba mkubwa wa Ngwair, David Mangwea
ambaye naye yuko Songea kuwa watu watakutanika Mbezi kwa msiba na pia mapokezi
yatafanyika Dar es salaam Mbezi Beach.
Taarifa zinaeleza zaidi kuwa ingawa
bado kikao cha familia nzima hakijafanyika lakini baba huyo mdogo amesema
wanaweza kulazimika kuzika Morogoro sehemu ambayo baba yake alizikwa.
Baba mdogo wa marehemu alisema
kuwa tayari ndugu wameshaanza kufanya taratibu za kuwasiliana na Ubalozi
wa Tanzania Afrika ya Kusini ili kujua ni jinsi gani mwili huo utafika hapa
nyumbani.
Naye msanii wa muziki huo, Moses Bushagama ‘Mez B’ mwili wa marehemu ulikabidhiwa jana
kwa Watanzania ambao wanaishi nchini humo.
“Bado hatujapata taarifa kamili
kuhusu kuletwa kwa mwili wake, lakini leo (jana) wanaukabidhi kwa Watanzania
ambao wapo huko, binafsi bado siamini kama ‘mshikaji’ ametutoka hadi niuone
mwili wake,” alisema Mez B.
Naye msanii wa muziki huo, Mbwana Mohammed ‘Mb Doggy’ alisema
Ngwea alikua ni msanii bora nchini na hakuna atakayeweza kuziba pengo lake,
tumuombee apumzike kwa amani.
“Kinachotakiwa
ni kumuombea mwenzetu apumzike kwa amani hiyo ni mipango ya mungu, leo kwake
kesho kwa mwingine,” alisema Mb Doggy.
Juhudi
za kumtafuta rafiki yake wa karibu, ambaye pia ni msanii wa muziki huo, Khalid
Mohamed ‘TID Mnyama’ ambaye alikua ni mtu wa mwisho kuongea nae ziligonga
mwamba baada ya kusema hawezi kuzungumza lolote kuhusiana na msiba huo kwani
bado haamini kama kilichotokea ni cha kweli.
No comments:
Post a Comment