HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 03, 2013

MAGUFULI ATAKIWA KUSAFISHA TANROAD

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Ujenzi John Magufuli, ametakiwa kukomesha vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wasiowaaminifu wa Mamlaka ya Barabara Tanzania (TANROADS), vya kuuza maeneo ya hifadhi ya barabara kwa wafanyabishara kinyume cha sheria.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Diwani wa Kata ya Saranda, Efraim Kinyafu alisema watendaji hao wamejihusisha na vitendo hivyo katika maeneo ambayo yametakiwa kuwa wazi kwa ajili ya upanuzi wa Barabara Kimara hadi Mbezi.

Alisema vitendo hivyo vinavyofanywa na watendaji hao vya uuzaji wa maeneo hayo, wakishirikiana na wenyeviti wa Serikali za Mitaa vimekuwa vikisababishia hasara kw wafanyabiashara pamoja na watu wengine mara sheria inapofuata mkondo wake.

Kinyafu alisema baadhiya wafanyabiashara walioangukia kwenye mtego huo ni wale waliondolewa kwenye maeneo ya Suka na Stop Over ambao baadhi yao wameuziwa ama wamepewa maeneo mengine kinyemela kwa maslahi ya genge la walanguzi, bado kisheri hayaruhusiwi kuendesha shughuli zozote za kibinadamu.

“Kwa mfano kuna tukio la wakazi wa Kimara ambao waliuziwa eneo la hifadhi ya barabara kinyemela na watendaji hao, kwa ajili ya ujenzi Msikiti kitendo ambacho baadaye kimeleta mtafaruku baada ya msikiti huo kutakiwa kubomolewa kwa kuwa ulijengwa kwenye hifadhi ya barabara”alisema Kinyafu.

Akizungumzia mgogoro uliyozuka kati ya wafanyabiashara hao wa Kimara na TANROADS, pale walipotakiwa kuondoka pembezoni mwa barabara ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo, Kinyafu alisema kwa kiasi kikubwa mgogoro huo ulichangiwa na uzembe wa wenyeviti wa serikali za mitaa kutokana na kuchelewesha barua zilizokuwa zikiwataka wafanyabiashara hao kuondoka kwa zaidi ya wiki tatu.

Alisema baada ya TANROADS kuamini kuwa barua hizo ziliwafikia wafanyabiashara hao, ilifika katika eneo husika kwa ajili ya kazi ya ujenzi wa barabara hata hivyo ilishangazwa ilipowakuta wakiwa bado wapo hivyo kutokuwa na njia nyingine zaidi ya kubomoa vibanda vyao hali iliyozusha mtafaruku.


Aidha, Kinyafu aliitaka serikali kuhakikisha inawatafutia maeneo ya kudumu wafanyabiashara hao ili kuepuka misuguano ya mara kwa mara isiyokuwa na sababu, na endapo watashindwa kufanya hivyo atawaagiza wandelee kufanya biashara zao katika maeneo wanayodhani wanaweza kujipatia wateja kirahizi.

No comments:

Post a Comment

Pages