HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 01, 2013

Nchi hii,Watuhumiwa Waharifu Wanapongezwa?

Na Bryceson Mathias
KATIKA Serikali ya aina yoyote duniani, Jamii, Madhehebu ya Dini, Asasi za Kiraia na Vyombo mbalimbali vya kutetea Haki za binadamu, hakuna anayeweza kumpongeza au kumtunuku mtu ambaye anatuhumiwa kufanya Uharifu.
Hatua hiyo haifikiwi hivyo kwa sababu, Pongezi hutolewa kwa mtu, Kikundi au Taasisi ambayo imefanya vizuri katika utendaji wake kutokana na Ueledi, Uadilifu na Uwajibikaji wa kile anachokifanya, anachokiongoza, na kukitekeleza kwa wakati muafaka na gharama nafuu.
Lakini katika siku za hivi karibuni, wananchi waliohojiwa kwa nyakati tofauti, wameanza kushangazwa kuona kwamba, kuna watu miongoni mwetu wanapata Tuzo za aina mbalimbali, Ijapokuwa, wengi wanaopongezwa, wana tuhuma za uharifu.
Nyakati hizi, Utashangaa Mtu au Mfanyakazi Umma, anafanya ubadhirifu mkubwa wa fedha au Rasilimali za Umma katika sehemu ya Kazi, lakini atapewa Tuzo, Cheo au Uhamisho kwenda sehemu nyingine ili akaharibu na huko, Ingawa uovu wake unafahamika.
Mtu akiharibu na kufuja mali ya Umma na kumhamishia mahali pengine, ni sawa sawa na kumtunuku Cheo au kumpongeza kwa alichoharifu, Jambo ambalo wengi wa wananchi wanahoji Je, anapongezwa kwa Uharifu ule aliofanya ili aendelee kufanya?.
Mfano; wananchi wanasema baadhi ya Wakurugenzi wa Wilaya nchini, wamebainika na Ofisi ya Ukaguzi wa Serikali nchini (CAG), kwamba wamefuja au kulipa Wakandarasi malipo hewa kwa kazi ambazo hawakufanya, na kukataliwa na Mabaraza ya Madiwani wao.
Lakini cha kusikitisha, badala ya kuchukua hatua na kutakiwa kurejesha au kulipa walichoharifu, wamepata tuzo za pongezi au vyeo ili waendeleze kuliharifu Taifa kwa Tabia zao zinazohojiwa na wananchi.
Katika Wilaya ya Mkulanga kwa mfano; baadhi ya Walimu wamelalamikia Kitendo cha Walimu wenzao wawili, waliokuwa Wakuu wa Shule za Sekondari, na kufuja Mamilioni ya Fedha za Ujenzi wa Nyumba za Walimu, Ada na Michango ya Serikali, kuhamishiwa Shule zingine.
Pia wamelalamikia Upendeleo uliofanywa kwa Walimu wenye Makosa hayo hayo kupewa adhabu mbili, kushushwa Ualimu Mkuu na kuwa Walimu wa Kawaida, wakifuatiwa na Uhamisho kwenda Mahali pengine. Je tuna sababu ya kuwapongeza waharifu hao?
Kufafanua Malalamiko hayo yanayoainisha karibu Mil. 66/- zimetumiwa vibaya katika Ujenzi wa Nyumba za Walimu, Mkurugenzi Wilaya ya Mkulanga, Saada Mwaluka, alisema, Mimi ni Mgeni wilayani hivyo sifahamu chochote kuhusu madai hayo, Ila nitafuatilia”.
Afisa Elimu Vifaa wa Wilaya, Mussa Ally, alipohojiwa na Mwandishi wa Makala hii, alikanusaha kupotea Mil. Sita kwa ajili ya Ujenzi wa Nyumba za Walimu pekee, ila alikiri fedha hizo ni za Ujenzi wa Nyumba za Walimu, Ada na Michango mbalimbali.
Kuhusu kushushwa Vyeo kwa Walimu na Uhamisho uliofanyika, alidai unatokana na Waliokaimu nafasi hizo kushindwa kuonesha Uwezo wao na mashirikiano na Halmashauri, ambapo kila mmoja wao ana Jambo la kujibu kutokana na Wakaguzi kutaka wajibu hoja.
Hivi karibuni Kamanda wa Polisi Iringa, Michael Kamuhanda, alipandishwa Cheo ingawa alilalamikiwa sana na kutuhumiwa kupelekea Mauaji ya Daudi Mwangosi. Pamoja malalamiko hayo, amepandishwa Cheo pamoja na Tuhuma alizotuhumiwa.
Aidha katika Biblia Takatifu Mungu anasema hivi, “Mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali. Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda” (2tim.2:5-6). Familia ya Mwangosi ilikuwa iwe ya kwanza kutunukiwa.

No comments:

Post a Comment

Pages