Kiungo Cesc Fabregas wa Hispania kushoto, akitafuta mbinu za kumtoka Andrea Pirlo wa Italia katika fainali ya Euro 2012
RIO DE JANEIRO, Brazil
Baada ya jana kushuhudia mchuano wa miamba ya Amerika Kusini Brazil dhidi ya Uruguay, ulioisha kwa Brazil kuichapa Uruguay mabao 2-1, leo michuano hiyo inaendelea kwa Hispania kuivaa Italia, zote zikipewa nafasi sawa ya kutinga fainali ya michuano hiyo iliyoanza Juni 15 na itafikia tamati Jumapili Juni 30
MIAMBA ya soka barani Ulaya, timu za taifa za Italia na
Hispania, leo zinajitupa kwenye dimba la Estadio Castelao, jijini Fortaleza,
katika pambano kali la nusu fainali ya pili ya Kombe la Mabara 2013
inayoendelea nchini hapa.
Baada ya jana kushuhudia mchuano wa miamba ya Amerika Kusini
Brazil dhidi ya Uruguay, ulioisha kwa Brazil kuichapa Uruguay mabao 2-1, leo michuano hiyo inaendelea kwa Hispania kuivaa Italia,
zote zikipewa nafasi sawa ya kutinga fainali ya michuano hiyo iliyoanza Juni 15
na itafikia tamati Jumapili Juni 30.
Nusu fainali hii ni marejeo ya miamba hiyo, iliyoumana
katika fainali ya Mataifa Ulaya ‘Euro 2012,’ iliyopigwa Julai 1, 2012 kwenye
dimba la Olimpiki jijini Kiev, Ukraine, ambako Hispania iliichapa Italia kwa
mabao 4-0.
Wakati Italia ikifuzu hatua hii bada ya kushika nafasi ya
pili katika kundi A nyuma ya Brazil, Hispania imefuzu kama kinara wa Kundi B,
ikifuatiwa na Uruguay baada ya mechi tatu tatu za hatua ya makundi.
Safu ya ushambuliaji ya Hispania imeonesha uhatari, baada ya
kutikisa nyavu mara 15 huku mabeki wake wakiruhusu bao moja tu, katika mechi
zake tatu za ushindi.
Kwa upande wa Azzurri, licha ya washambuliaji wake kutisha
kwa kufunga mabao nane katika mechi tatu – ilikoshinda mbili na kufungwa moja,
safu ya ulizni ya kikosi hicho imeonesha udhaifu, baada ya kuruhusu mabao nane pia
katika mechi hizo.
Washindi wa nusu fainali ya jana na leo, wataumana katika
fainali kali Juni 30 kwenye dimba la Estádio do Maracanã, jijini hapa, kuwania
kitita cha dola za Kimarekani milioni 4.1, huku mshindi wa pili akilamba dola
milioni 3.6.
Aidha, timu zitakazofungwa katika hatua hii zitaumana mapema
Juni 30 hiyo hiyo kwenye Uwanja wa Arena Fonte Nova, jijini Salvador, kuwania
zawadi ya tatu ya dola milioni 3, huku mshindi wa nne akiambulia dola milioni
2.5.
Kabla ya nusu fainali ya kwanza jana usiku, mshambuliaji
Fernando Torres wa Chelsea, alikuwa akiongoza mbio za Kiatu cha Dhahabu cha
michuano hiyo ya kwanza kabisa kutumia Teknolojia ya Goli (Goal Line Technology
- GLT), akiwa na mabao matano.
Supersport.com
No comments:
Post a Comment