BAADA ya Kifo cha Muasisi na Mpigania wa Uhuru wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kama ilivyokuwa wakati wa Kifo cha Yesu Kristo, yaliyotokea haya!
“Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka. Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza;
Wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi? Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno.
Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu”. Marko 16:3-5
Toka mwenye uchungu na nchi hii (Nyerere) aondoke, nchi iliingia kugandamizwa na jiwe kubwa la uuzwaji wa viwanda, Biashara huria, uwekezaji uchwara, madawa ya kulevya, mauaji yaliyokithiri, Rushwa na Ufisaji Mkubwa; tunajiuliza, ni ani atakayetuvingilishia Jiwe hilo?
Biblia inasema, “Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka. Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza”
Mbona sisi siku za uchaguzi kwenye sanduku la kura alfajiri, tunapiga kura za kukumbatia na kustawisha Rushwa, Madawa ya Kulevya yanayoathiri na kuua watoto, wizi na utoroshaji wa Rasilimali zetu, Madawa na bidhaa feki, na hatimae Ufisadi uliokubuhu viendelee?.
Wale akina mama wanne, walisemezana wao kwa wao na kumtafuta nani atakayewaondolee lile jiwe mlangoni ili waone maisha Bora kwa kila mtu yaliyokuwa yakipatikana kwa kumuona Yesu, japo alikuwa kaburini alikuwa na nguvu na uwezo huo.
Leo hii, Taasisi na Asasi za Dini, Wanaharakati, Vyombo vya Haki za binadamu, Wanasheria, Wanasiasa, Wabunge, Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa na Mtanzania mmoja mmoja wenye uchungu na nchi hii wakiwemo Wana habari, mnasemezana nini?
Bibilia katika kitabu cha pili cha Wafalme 13:20 inasema, “Elisha akafa, nao wakamzika. Basi vikosi vya Wamoabi wakaingia katika nchi mwanzo wa mwaka.
“Ikawa, walipokuwa wakimzika mtu, angalia, waliona kikosi; wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisha; mara yule maiti alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka, akasimama kwa miguu.
Naamini Tanzania wapo watu wenye mifupa yaani Roho, Elimu, Ujuzi, Hekima, Maadili, Uchungu, Upendo na Ueledi wa Usia na Chembechembe za Nyerere na Edward Moringe Sokoine, wanaoweza kuifufua nchi kama ilivyofanya mifupa ya Elisha kwa ile maiti.
Ili kuondokana na Jiwe kubwa la Rushwa, Ufisadi, Kodi za Simu, Madawa ya kulevya, Dhuluma, Mauaji, Maisha magumu kwa kila sekta (Wafanyakazi wa taasisi binafsi na za Umma, Walimu waliokata tamaa, Wakulima, Wafugaji na wengine;
Dawa na Mfupa wa kwanza utakaofufua matumaini mapya ya Taifa letu, ni kwenye sanduku la kura 2014 kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa, na 2015 kwenye Uchaguzi Mkuu kwa wale ambao Mungu atakaowachagua kuuona mwaka! Narudia, Suluhisho ni Sanduku la Kura.
Lakini Dawa na Mfupa wa pili ni taasisi za Haki za binadamu, Wanaharakati, Vyombo vya Sheria, na mtu mmoja mmoja katika eneo hilo, waumizwa na hali hii, wasimame pamoja ili kulikomboa Taifa hili kwenye ukoloni huu mkongwe wa pili.
Tumeshudia watuhumiwa wa madawa ya kulevya Wanakamatwa; lakini wakihukumiwa wanakata rufaa, na huko kwenye rufaa ndiko rushwa na ufisadi unatembea, siku mbili wanaachiwa unawaona mitaani, na watoto wetu wanaendelea kuumia na hatimae wanakufa.
Tumemsikia Rais Jakaya Kikwete akiwaamuru wakimbizi na Wageni waliojipenyeza nchini bila utaratibu maalum, warudi makwao! Na kwamba wasipofanya hivyo! Watasakwa na kurudishwa kwa nguvu. Ni wangapi wamejificha nchini? Nani anawajua? Hakuba.
Lini watanzania sasa, tutatumia sanduku la kura kama Malaika wa kutuondolea jiwe, kurudisha heshima yetu kwa kuwaondoa wageni wanaopora Rasilimali zetu kwa uwekezaji uchwara unaoitwa mikataba ya siri?
Siri gani zinazofanywa ndani ya nchi yetu sisi tukiwemo? Biblia inasema Siri zote ni za Mingu.
“Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.“Kumbukumbumu la Torati 29:29.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715-933308
No comments:
Post a Comment