HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 04, 2013

Wahanga wa Mafuriko Kilosa wadai kutishiwa Maisha

Na Bryceson Mathias, Morogoro
 
VIONGOZI wa Wahanga wa Mafuriko ya Maji Kilosa, Mathey Gervas, na Nashon Salehe, wameilalamikia Serikali kuu kuwa wanatishiwa maisha na watu wasiowafahamu, kutokana na wao kuhoji ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kuwapatia makazi ya Kudumu.
 
Wakizungumza na Tanzania Daima jana [4.6.2013] toka Mafichoni Wahanga hao walisema, kilichosababisha waanze kufuatwa fuatwa na kutishiwa maisha, ni baada ya taarifa za malalamiko yao kuripotiwa na Radio ya Jamii Kilosa,
 
Viongozi waliotishiwa ni pamoja na Mwenyekiti Salehe wa maeneo yote yaliyoathirika, Mazuria, Kimamba, na Kondoa, na alipohojiwa toka alipojificha alikiri kufuatwa fuatwa usiku nyumbani kwake na watu asiowafahamu, huku wakimtishia maisha kwa nini anahojihoji ahadi ya Rais, lini atawapatia makazi ya kudumu.
 
“Wanakuja usiku nyumbani kunibishia hodi, na ninapotaka wajitambulishe ni akina nani, huwa hawataki kujitambulisha zaidi ya kunitaka nifungue mlango, na nikisema sifungui wananitishia kuwa maisha yako yamo hatarini, wewe na mwenzako Geervas”.alisema Salehe huku akisema ukitaka ubaya nchini dai haki yako!
 
Salehe alisema, watu hao wanadai maswali tunayowahoji kuhusu ahadi ya Kikwete kwa Wahanga wa Kilosa si ya kwetu, wandai labda tumefundishwa na baadhi ya wanasiasa wanaokinzana nao au pengine tumefundishwa na wanaharakati walio kinyume nao.
 
Aidha Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Eliasi Tarimo, alipigiwa simu ya kiganjani ili kutoa ufafanuzi alikanusha kwa njia ya ujumbe mfupi akisema,
 
“Hakuna ukweli wowote katika madai hayo. Nao,ba nikuulize. Serikali inaweza kutisha wananchi wanapodai haki yao? Naomba uje ofisini upate ukweli kuhususuala la Wahanga na hatua ambayoSerikali imeshachukua ikiwa ni pamoja na kuwaandalia Viwanja vya Kujenga”.
 
Wilaya ya Kilosa na hasa Ruaha, imekuwa na Mvutano mkubwa baina ya Vyama Vikuu vya siasa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, ambapo baadhi ya Viongozi chadema wapo ndani, kwa kinachoelezwa uharibifu wa Mali.

No comments:

Post a Comment

Pages