Zuberi Mussa katika mwonekano wa picha tofauti
tofauti nje ya Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mazinde.
Zuberi Mussa (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Mwandishi Dotto Mwaibale (kushoto), Mashaka Kibaya (kulia) wote wa Gazeti la Jambo Leo na Mashaka Mhando wa Gazeti la Majira mkoani Tanga, walipokwenda kumjulia hali kijjiini kwao.
Na Dotto Mwaibale, Tanga
Zuberi Mussa ambaye ni mpiga picha mkongwe katika vyombo mbalimbali vya habari nchini ambaye kwa sasa anafanyakazi Kampuni ya New Habari ni mgonjwa anayehitaji msaada wa hali na mali.
Kikubwa kinacho msumbua mwandishi mwenzetu huyu ni ugonjwa ambao bado haujafahamika ambapo kwa mtu anayemfahamu ni rahisi kumgundua kuwa ana matatizo ya kiafya kwani katika kila sentesi yake ya pili na ya tatu wakati wa kuongea naye hautaelewana naye kutokana na matamshi yake ambayo hayafahamiki yanayoonesha kama mtu aliyechanganyikiwa.
Kutokana na kukosekana kwa fedha za kumsaidia katika matibabu hasa Hospitalini, Zuberi Mussa amelazimika kwenda kupata matibabu yake kwa waganga wa jadi.
Wakati Zuberi akiwa kijijini kwao Kata ya Mazinde wilayani Korogwe mkoani Tanga bila ya kuwa na msaada wowote mke wa mwenzetu huyo aitwaye Rehema Amir kwa kipindi cha mwaka mzima yupo hoi kitandani kutokana na maradhi ya kupooza yaliyompata mwanzoni mwa mwaka jana akiwa jijini Dar es Salaam, hawezi kufanya chochote ikiwa ni pamoja na kuongea hakika inaumiza na kusikitisha.
Ndugu wanahabari kila mmoja wetu kwa imani yake na utamaduni tulionao wa kusaidiana tujitokeze kumsaidia mwenzetu huyu ambaye anapita katika kipindi kigumu.
Binafsi nilipofika kumuona kwa mara ya kwanza wiki iliyopita nilishitushwa na hali aliyokuwa nayo ingawa kaka yake aitwaye Waziri Mussa anayemuuguza alidai kuwa alikuwa amepata nafuu.
Zuberi alifika katika eneo nililokuwepo akiwa katika hali ambayo si ya kawaida zaidi ya kusalimiana na kunitambua mengine yote nilioongea naye hatukuweza kuelewana. Kwa mtu yeyote atakayependa kumsaidia Zuberi pamoja na mke wake kipenzi Rehema Amir anaweza kuwasiliana na Dotto Mwaibale kwa namba 0712-727062 ambaye atakuunganisha na kaka yake.
Ndugu wanahabari wenzangu na mtu mmoja mmoja, Taasisi yoyote, shirika lolote, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Wafanyabiashara, Makampuni mbalimbali na vyama vya michezo hima tujitoe kimasomaso kumsaidia mpiga naji mwenzetu Zuberi Mussa na mke wake waondoke katika matibabu ya jadi wanayopata kwa waganga wa kienyeji badala yake wapelekwe hospitali kwa uchunguzi zaidi wa afya zao kwani kutoa ni moyo na si utajiri.
Mwenyezi Mungu awasaidie wapate msaada katika kipindi hiki kigumu. Poleni sana.
ReplyDeleteI.A. Mwaipaja