Na Francis Godwin, Ludewa
MBUNGE wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe Deo Filikunjombe (pichani), ameeleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya wabunge ambao wanaongoza kwa kusinzia bungeni badala ya kuwawakilishi wananchi wao na kuwa yeye si mbunge wa kulala bungeni .
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata ya Ilela na Manda wakati wa ziara yake ya kusherekea pamoja na wapiga kura wake sikukuu ya Krismas na Mwaka mpya juzi ,Filikunjombe alisema kuwa amekuwa bega kwa bega na wananchi ikiwa ni pamoja na kuwawakilisha vema bungeni bila kusinzia kama wanavyofanya baadhi ya wabunge .
Kwani alisema kuwa kazi ya uwakilishi wa wananchi ina hitaji kujituma na kuwajibika kwa hali ya juu na si tofauti na hayo na kuwa yeye kama mbunge kila mmoja amekuwa ni shahidi na kuwa hatakuwa tayari kukosolewa na wapiga kura wake eti kwa kusinzia bungeni ama kushindwa kuwatumikia vema.
Katika hatua nyingine mbunge Filikunjombe amewatoa hofu ambayo awali ilikuwepo kwa wananchi wa Mwambao kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi na kuwa mgogoro huo umekwisha na kuwayaka wananchi kuendelea nashughuli zao kama kawaida .
Alisema kuwa awali zilikuwepo taarifa kuwa Rais wa Malawi Joyce Banda kudai ziwa Nyasa lote ni mali ya nchi yake ya Malawi wananchi wa Tanzania wanaoishi jirani na ziwa hilo upande wa Tanzania walianza kuigiwa a hofu kubwa .
Mbunge huyo alipongeza jitihada kubwa zilizofanywa na serikali ya Rais Dr Jakaya Kikwete katika kumaliza mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi na kuwataka wananchi wanaoishi mwambao wa ziwa Nyasa kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.
Filikunjombe alisema kuwa serikali ya Rais Kikwete ni serikali sikivu na ndio sababu ya kulishughulikia suala hilo la mgogoro wa mpaka kwa wakati zaidi bila kutokea machafuko ya aina yoyote .
Mbali ya kuingiwa na hofu hiyo ya kiusalama ila bado walikuwa wakifanya shughuli zao kwa hofu kubwa na baadhi yao kushindwa kuwajibika vema katika shughuli za kimaendeleo kwa kuhofu vita kutokea .
Hata hivyo alisema kutokana na serikali ya Kikwete kuwa sikivu zaidi baada ya kubaini suala hilo mara moja jitihada za kulifanyia kazi hilo bila kumwaga damu ilianza kufanyika na kuwa kwa sasa Rais Kikwete amemaliza mgogoro huo na hakuna tatizo tena.
" Ninawahakikishia wananchi wangu wa Manda na Ilela pamoja na kata nyingine zote kama Makonde, Lifuma na zote ambazo zipo jirani na ziwa Nyasa na wanategemea maisha yao kwa kuvua samaki na dagaa katika ziwa hilo ....kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote" alisema mbunge Filikunjombe huku akishangiliwa na wananchi hao
Alisema kuwa Rais Kikwete amekuwa akijituma sana katika kuwatumikia watanzania ila wapo baadhi ya watendaji wa serikali ambao ni mzigo katika serikali yake na wamekuwa wakishindwa kuwatumikia wananchi vema.
Filikunjombe alisema yeye kama mbunge na mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Ludewa kamwe hatakubali kuona wananchi wake wanakosa huduma za msingi kama ilani ya CCM inavyosema kutokana na baadhi ya viongozi kushindwa kutimiza majukumu yao vema.
Alisema kuwa kwa kutumia fursa za ziwa Nyasa wananchi wa maeneo ya mwambao mwa ziwa hilo wanaweza kujikwamua kiuchumi kwa kupatiwa vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya uvuvi badala ya kuendelea kuifanya kazi hiyo kwa kutumia vitendea kazi duni na kufanya uvuvi wao kutokuwa na tija ya kimaendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake John Haule alisema kuwa awali walikuwa na hofu kubwa ya kuendelea kufanya shughuli za maendeleo kutokana na hofu ya kutokea vita ya mpaka kati ya Malawi na Tanzania na kuwa hata wakati mwingine wakiona ndege zikipita angani walikuwa wakiogopa kuwa yawezekana ni ndege za vita kutoka Malawi na zinataka kuwaangamiza.
"Tunakupongeza kwanza wewe mwenyewe mbunge wetu Deo Filikunjombe kwa kutuwakilisha vema kwa Rais Kikwete na bungeni pia tunataka kuwaeleza viongozi wa CCM sisi wana Ludewa tumechoka kuendelea kuwa na mbunge wa kipindi kimoja kimoja sisi kwa sasa hatuhitaji mbunge mwingine zaidi yako na kama watafanya wao watakavyo tupo tayari kuhama na wewe papote"
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ludewa Juma Madaha mbali ya kuungana na mbunge Filikunjombe kuwahakikishia usalama wananchi hao bado alisema kuwa ni vema wananchi hao kutumia mvua zilizopo kwa kulima mazao yanayohimili ukame kama mihogo ambayo imekuwa ikistawi zaidi katika maeneo hayo .
Kwani alisema kuwa wataalam wa hari ya hewa wanadai kuwa hali ya mvua kwa mwaka huu si nzuri sana pia upo uwezekano wa mwakani Taifa kutokuwa na neema kutokana na wataalam hao katika uzoefu wao kuonyesha miaka yote inayo malizika na namba 4 kuwa na tatizo la neema.
No comments:
Post a Comment