HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 24, 2023

Upatikanaji wa vifaa uliovyoongeza ufaulu wa wanafunzi wenye ulemavu mtihani wa Taifa Zanzibar

Baraza la Wawakilishi limepitisha sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2022 na kufuta sheria ya watu wenye ulemavu haki na fursa ya namba 9 ya mwaka 2006.

 

Sheria hii mpya imetoa fursa ya kuanzishwa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu ambalo miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia maendeleo ya watu wenye ulemavu kwa ujumla wake.

 



Sheria hiyo tayari imetiwa saini na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Bapinduzi na kuwa sheria kamili kwa ajili ya utekelezaji wake.

 

 

Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar limeelezea kuridhishwa na utekelezaji wa sheria hii mpya hasa katika sekta ya elimu.

 

 

Linasema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imewashirikisha kikamilifu wanafunzi wenye mahitaji maalumu kufanya mitihani ya taifa ikiwemo darasa la 4, 7, hadi kidatu cha pili kwa mafanikio makubwa.

 

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa baraza hilo, Salma Sadati Haji, alisema kuna ushirikishwaji mkubwa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika mitihani ya taifa iliyoandaliwa na  Baraza la Mitihani la Zanzibar. (BMZ).

 

 

Alisema miaka iliopita wanafunzi wenye mahitaji maalumu ikiwemo wenye ulemavu hawakushirikishwa kikamilifu katika kufanya mitihani yao kwa sababu mahitaji yao yalikuwa hayapatikani.

 

 

Alifahamisha matarajio yao ni kuona ujenzi wa shule za msingi na sekondari zinazoendelea zinazingatia mahitaji mahsusi kwa watu wenye ulemavu ili kufaidika na elimu inayotolewa nchini.

 

 

 

“Baraza la watu wenye ulemavu limefurahishwa na juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kutoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kuhakikisha nao  wanapata haki ya msingi ya elimu kwa wote,”alisema.

 

Akizungumzia wanafunzi wenye mahitaji maalumu waliofanya mitihani ya darasa la nne, la saba na kidatu cha pili, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ussi Debe Khamis, alisema wameridhishwa na maandalizi yalivyofanywa kwa wanafunzi wenye ulemavu na kufanya mitihani yao bila kizuizi.

Debe alisema  wanafunzi 819 walifanya mitihani iliyotayarishwa na Baraza la Mitihani la Zanzibar wakiwemo wenye ulemavu wa viungo, uoni hafifu, viziwi na walemavu wa akili.

 

 

Kwa mfano alisema katika mitihani ya darasa la nane jumla ya watahiniwa 362 walikuwa wenye mahitaji maalumu wakiwemo wasioona watatu,uoni hafifu 154, viziwi 51, walemavu wa akili 98, walemavu wa viungo 36 na walemavu wa mchanganyiko 20.

 

Aidha katika watahiniwa wa darasa la saba, wanafunzi wenye mahitaji maalumu 160 walifanya mitihani hiyo wakiwemo wasioona mmoja, uoni hafifu 60, viziwi 18, walemavu wa akili 54, walemavu wa viungo 21 na walemavu wa mchanganyiko sita.

 

 

Alifahamisha kwa upande wa watahiniwa wa kidatu cha pili, wanafunzi wenye mahitaji maalumu waliofanya mitihani walikuwa 297,ambapo wakiwemo asieona mmoja, uoni hafifu 187, viziwi 25, walemavu wa akili 52,  walemavu wa viungo 20 na  waliemavu wamchanganyiko 12.

 

 

 “Ukijumlisha na kufanya hesabu utapata jibu la jumla ya watu wenye mahitaji maalumu 819 waliofanya mitihani yao huku wengi wakipata ufaulu unaoridhisha,”alisema.

 

 

Aidha Debe alionesha kufurahishwa na mwamko wa wazazi kuonesha utayari wa kuwapeleka watoto wao shule kupata elimu na kuondokana na dhana kwamba ni “mzigo” na kuwabakisha nyumbani.

 

 

Alizitaja changamoto kubwa ziliopo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika kupata elimu kuwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kusomeshea na walimu wenye sifa na ujuzi wa kusomesha wanafunzi wenye mahitaji maalum.

 

 

Kwa mfano alisema hadi sasa shule nyingi ambazo wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapata elimu hazina vifaa vya kutosha vya kujifunzia.

 

 

 

“Changamoto ya vifaa vya kufundishia bado ni tatizo kubwa ambapo unafika wakati shule moja ina  mashine moja tu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kutoona, mazingira kama haya yanakuwa magumu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum,” alisema.

 

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwanakheiri Adam Ameir, alisema wizara ipo katika mageuzi makubwa ya sekta hiyo ili kuhakikisha makundi yote wakiwemo watu wenye ulemavu wanapata fursa ya elimu kwa mujibu wa sheria na na mikataba ya kimataifa.

Alizitaja juhudi zinazotarajiwa kuchukuliwa na Wizara ni pamoja na ujenzi wa shule zote kuwa na huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

 

 

Adil Mohamed Ali,  Mratibu wa Chama cha Wasioona Zanzibar, ZANAB, alisema changamoto zinazowakabili watu wasioona ni kubwa ikiwemo upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya kufundishia wanafunzi.

 

 

 “Yapo mafanikio makubwa yamefikiwa kwa upande wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika kuwapatia elimu wanafunzi wenye mahitaji maalum ikiwemo kufanya mitihani yao lakini upatikanaji wa vifaa unahitaji kuangaliwa upya,” alisema.

 

 

 “Katika sheria mpya ya watu wenye ulemavu inatutaka kuhakikisha majengo yote ya shule yanakuwa na sifa na viwango kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kufaidika na fursa za elimu zinazotolewa,”alisema.

 

 

Fatma Issa Haji, mwanafunzi wa kidatu cha pili aliefanya mtihani katika shule ya Marumbi Wilaya ya Kati na kufaulu alizitaja changamoto za uhaba wa vifaa vya kufundishia kama kikwazo cha kushindwa kufaulu kwa kiwango cha juu.

 

 

 “Nimefanya mtihani na kufaulu vizuri lakini zipo changamoto nyingi zinazotukabili ikiwemo ukosefu wa walimu wenye uwezo wa kufundishia wanafunzi kama sisi viziwi,”alisema.

 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman, ambaye anashughulikia watu wenye ulemavu alisema wamejipanga kuhakikisha sheria mpya ya watu wenye ulemavu inatekelezwa na kusimamiwa kikamilifu.

 

 

Alisema sheria hiyo imetoa haki na fursa nyingi ikiwemo za ajira serikalini na sekta binafsi.

Alisema lengo la sheria mpya ni kwenda na wakati wa mabadiliko yaliopo sasa ya dunia ikiwemo mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo inalinda haki za makundi hayo.

 

“Miongoni mwa marekebisho makubwa ya sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2022 yaliyofanywa ni kuona kundi hilo linanufaika na kupata haki ya msingi ya elimu kwa kufaidika na fursa zote zilizopo kwa mujibu wa sheria bila ya kubaguliwa pamoja na ajira katika sekta mbalimbali kwa watu wenye ulemavu wenye sifa,”alisema.

 

 

Mwanaharakati Asha Aboud akitoa elimu kwa waandishi wa habari kuhusu kuripoti matukio na taarifa za makundi yaliopo pembezoni wakiwemo watu wenye ulemavu, wanawake na watoto katika mafunzo yaliyotayarishwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa-Zanzibar) kwa ufadhili wa  Foundation for Civil Society  (FCS), aliwataka kubainisha changamoto zote zinazowakabili ili serikali ichukue hatua za utekelezaji.

 

 

 “Miongoni mwa majukumu yenu waandishi wa habari ni kwenda kuibua changamoto mbalimbali zinazoyakabili makundi ya jamii yaliopo pembezoni ambayo yanakabiliwa na matatizo mengi kiasi ya kushindwa kutekeleza majukumu yao,”alisema. 

 

 

Ujenzi wa shule za Pujini kwa upande wa Pemba na Jendele kwa Unguja ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na serikali kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapata haki na fursa sawa za elimu ya ujasiriamali ambayo itawawezesha kujiajiri.

 

No comments:

Post a Comment

Pages