LICHA ya timu ya Simba, kukubali kichapo cha mabao 3-0
dhidi ya Zesco katika mchezo wa sherehe yao ya ‘Simba Day’ mwishoni mwa wiki
iliyopita, uongozi wa timu hiyo, umesema haujaumizwa na matokeo hayo kwa kuwa
timu bado inaandaliwa.
Simba waliumana na Zesco katika uwanja wa Taifa Jijini Dar
es Salaam Jumamosi ya wiki iliyopita, huku wanachama na mashabiki wa Simba
wakijitokeza kwa wingi kuona usajili wao mpya wa kikosi chao.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange
‘Kaburu’ ambaye alizungukwa na mashabiki kibao mara baada ya kumalizika kwa
mchezo huo, alisema, timu yao ni nzuri ila tatizo lilofanya mpaka wapoteze
mchezo huo ni kutokana na timu kutokuwa pamoja kwa muda.
Kaburu alisema, wachezaji wao bado hawajaelewana, ila kwa
kuwa wanaenda kambini Zanzibar kwa wiki tatu anaimani kubwa wakirejea watakuwa
wameelewana na kufanya vema katika mechi zijazo.
Alisema, mfano katikati alikuwa akicheza Shabani Kisiga na
Pierre Kwizera hawajawahi kucheza pamoja na hiyo ni mara ya kwanza, pia Raphael
Kiongera na Hamis Tambwe, pamoja na Abd Banda na Donald Musoti.
“Timu yetu iko vizuri mno, na siku za usoni wanasimba
wataifurahia sana, kwa kuwa wachezaji wetu wengi wapya hawajazoeana kama
nilivyosema hapo awali, lakini watapata muda tu huko Zanzibar na watafanya
vizuri,”alisema Kaburu.
Aidha Kaburu aliongeza kwa kuwataka wapenzi wa Simba na
wanachama, kutoikatia tamaa timu yao kupitia mchezo huo mmoja tu, na wao kwa
kuwa walihitaji ushindani ndio maana wakaichukua timu inayoshika nafasi ya pili
katika ligi nchini kwao.
No comments:
Post a Comment